Jinsi ya kujipatia pesa,huku ukifurahia maisha!

Njia tatu za kugeuza ujuzi wako uwe pesa.

Hivi si ni kama maisha yanazidi kuwa magumu eh? Vitu mtaani bei ghali halafu mfukoni huna hata shilingi,Sasa kama Msichana unafanyaje?

Jamani, kina dada mnaonaje tukiwa wabunifu. Hata kama huwezi kutoka na kwenda kujitafutia kazi, fikiria kuhusu mambo yale ambayo unaweza kuyafanya vizuri sana na uweze kulipwa kupitia mambo hayo.

Mahanjumati ya Martha

Je, wewe uko vizuri kwenye mapishi? Je marafiki zako wamewahi kuonja chakula chako wakakisifia,na siku zote hutamani kula wanapojua kwamba wewe ndiwe uliyepika? Basi anza kuuza vyakula au vitafunwa shuleni ulivyoandaa nyumbani. Martha ana umri wa miaka 13 na amekuwa akimsaidia mama yake kupika tangu akiwa mdogo sana. “Kila ninapohitaji hela ya mfukoni huwa natengeneza keki halafu naziuza tukitoka darasani. Huwa ninaziuza keki zangu kwa bei ya chini kushinda zile zinazouzwa kwenye dukani pale shuleni, na huwa ziko freshi kwa hiyo watu wanazipenda mno.”

Maria Anafundisha twisheni Maria ana miaka 16 tu, lakini tayari yeye ni mwalimu kwa sababu akitoka shuleni anawafundisha watoto watatu wanaoishi karibu na nyumbani kwao. Alianza kama utani vile, kwa kuwasaidia watoto wa majirani zake walipokuwa wanamwomba msaada, lakini baadhi ya wazazi walifurahishwa sana kwa jinsi binti zao walivyokuwa wanaelewa haraka kiasi kwamba waliamua kumlipa kwa kuwasaidia watoto wao katika kazi zao za shuleni mara mbili kwa wiki. Maria anasema, Ukitoa kwa wengine uliyojifunza kutokana na kujisomea, basi mema yatakurudia. “Ninapata hela za kununulia vitu ninavyovipenda, na ninajisikia vizuri kwa sababu ninajua ninamsaidia mtu mwingine kujifunza pia.”

Kazi Ya Uchoraji Ya Halima

Halima kwa sasa ana miaka 18, lakini alianza kusanifu nembo na mabango kwa ajili ya biashara hapo mtaani kwake tangu alipokuwa na miaka 15. Anasema, “Ikiwa unapendelea sana mambo ya uchoraji, watu wengine watakushangaa Uchoraji?Hebu tafuta vitu vya maana vya kufanya”. Halima anasema unadhani nani anachora picha zote wanazohitaji wafanyabiashara? Picha hazijichori zenyewe, huchorwa na watu!"

Halima alianza kwa kuchora picha na kwa kutumia sanaa ya kompyuta kumtengenezea shangazi yake tangazo la biashara yake ya saluni. Shangazi yake alifurahia sana kazi kiasi kwamba alimuunganisha Halima kwa marafiki zake wawili waliokuwa wafanyabiashara wachanga. Baada ya muda mfupi,Halima alipata wateja kutoka mjini kote na sasa anasomea usanifu wa picha.

Je, wewe una kipaji au ujuzi gani?. Pengine inaweza kukuletea pesa.

Share your feedback