Kubalehe kulinitokea mapema.

Mambo, naitwa Aisha. Nakumbuka nilipokuwa mdogo, nilikuwa na shauku kubwa ya kuwa mkubwa. Nakumbuka kipindi ambacho nilikuwa napenda kukaa kupiga stori nikiwa na dada yangu na marafiki zake.Kuna wakati nilikuwa najisikia vibaya vile watu walikuwa wakiniambia mimi bado mdogo sana. Binafsi wala sikuwa najiona mdogo kihivyo,nilikuwa najiona nimeshakuwa mdada.

Nadhani nilianza kuongea mapema sana pia, kwa sababu kukua si rahisi kama inavyoonekana. Huja na hatua muhimu katika maisha ambayo ni Ubalehe. Ubalehe ni wakati miili yetu inaanza kupitia mabadiliko kadhaa .Kwa wasichana, hii humaanisha maziwa kukua na nyonga kutanuka , kuanza kuota vinyweleo kwenye mikono na miguu. Lakini pia ni kipindi ambapo homoni zetu zinapoanza kufanya kazi. Kipindi hiki kinaweza kuanza katika umri wowote kati ya miaka 8-15, lakini kwangu nilibalehe mapema zaidi, hii hali ilikuwa ngumu kwangu kukabiliana nayo.

Nilianza kuona tofauti pale ambapo watoto wengine walipoanza kunisema kuhusu mwili wangu. Waliniongelea maneno mabaya kama vile "uso wako upo kama stafeli" ama "kwanini una maziwa makubwa hivyo kwani wewe ni mjamzito"?

Kitendo cha kuwa wa kwanza kuvunja ungo kilinifanya nijisikie wa ajabu. Sikuwa nafurahia maneno waliyokuwa wakiniambia hivyo niliamua kumweleza mama yangu kwani ninamuamini.

Mama yangu alinifariji sana. Aliniambia niyapuuze maneno yote waliyokuwa wakiniambia. Alinifundisha kuwa Ubalehe ni kitendo cha asili katika hatua za ukuaji kwa wasichana na wavulana na sipaswi kujisikia aibu kutokana na kuwahi kubalehe kuliko watu wengine.

Ni kweli kwamba inaweza ikawa ni kitu cha ajabu lakini kiujumla ni kipindi kizuri cha mabadiliko chanya. Aliniambia hakuna mtu mwenye haki ya kunitania kuhusu mwili wangu.

Nikijaribu kutazama nyuma,kuhusu hili lililonitokea nagundua kuwa maamuzi ya kuzungumza na mama yangu yalikuwa ni maamuzi sahihi mno.Kitendo cha kumueleza mabadiliko niliyokuwa nikiyapitia kilinifanya nijawe na ujasiri na kutokuwa na aibu tena.Kwa vile niliwahi kubalehe, hii imeweza kunisaidia kuwaongoza wengine katika safari zao.Ukweli ni kwamba katika kila jambo baya kuna upande ambao ni mzuri.

Kama upo kama mimi na umebalehe mapema, jaribu kutokuficha hisia zako. Jaribu kumtafuta mtu unayemuamini, inaweza ikawa jirani yako, mwalimu wako, au rafiki yako na jaribu kuzungumza nao kuhusu jambo hili. Kuvunja ukimya kunaweza kukusaidia kufurahia safari yako ya ubalehe. Kumbuka, kila mmoja hupitia hatua hizi hatupaswi kupitia uzoefu huu peke yetu.

Share your feedback