Ubunifu unaweza kuongeza kujiamini
Maisha sio rahisi toka wazazi wangu walipofariki. Nilikuwa mtoto wao wa pekee na walikuwa kila kitu kwangu. Kuwapoteza wazazi wangu nilijisikia nimebaki pekee yangu, pasipo mlezi wala msaada- hasa pale ninapohitaji kufanya maamuzi, ama kuhitaji ushauri, na zaidi hasa pale ninapohitaji msaada wa kifedha.
Nilichukuliwa na shangazi na mjomba, ambao walinitunza kama mtoto wao. Ninawashukuru mno kwa msaada na upendo wao. Walikuwa wakarimu mno kwangu, ila nilikuwa nikiona tabu kuwategemea kwa kila kitu, sikuwa na ujasiri kuhusu hili, na hata wakati mwingine nilijisikia kama hatia, hasa pale ukizingatia walikuwa na Familia waliyopaswa kuihudumia.
Siku moja mchana rafiki yangu alinitembelea na tulikuwa tukisukana jikoni. Napenda kusuka nywele zangu na huwa natumia nywele za rafiki zangu kujifunzia kusuka mitindo mbalimbali, na hii inaonekana kuwa moja ya hobi inayonivutia sana. Shangazi aligundua kipaji changu na akanishauri kutumia hobi yangu kama sehemu ya kujiingizia kipato. Alitambua jinsi nilivyokuwa nikijisikia na alitaka kunisaidia.
Sikuwahi kufikiria hapo mwanzo kama ningeweza kugeuza kitu nilichokuwa nakipenda na kuanza kujitengenezea kipato. Nilikuwa na shauku kubwa ya kujaribu kufanya. Shangazi alinisaidia kutengeneza matangazo ili kuitangaza biashara yangu hii na alinipa sehemu ya kufanyia kazi za ususi kwenye nyumba yake.
"Mungu si athumani" siku za mwisho wa wiki nikaanza kuwa bize kuikuza biashara yangu hii mpya, nilihakikisha najitahidi kuwahudumia vizuri wateja wangu wachache wa mwazo waliojitokeza, kadri ilivyowezekana. Watu walinisaidia kuitangaza biashara na baada ya muda watu wakaanza kuongezeka.Kufumba na kufumbua nikawa msusi maarufu sana mjini.
Toka wakati biashara yangu ilipo anza kuchanganya nilianza kuwa jasiri kuhusu maisha yangu na hata siku za baadae. Kuwa na pesa niliyoitolea jasho mwenyewe na ambayo nilikuwa na uhuru wa kuitumia nilivyopenda ilinifanya niwe huru na imenifanya nijitegemee kama nilivyokuwa natamani hapo mwanzo.
Share your feedback