Kufuata ndoto zangu

Kuleta uadilifu kwenye maonyesho ya urembo

Maonyesho ya urembo ni taaluma ya kuheshimika kwa wasichana katika nchi nyingi. Hiki ni kisa cha msichana mmoja.

Jina langu ni Aurore na ninaishi nchini Rwanda. Tangu nilipokuwa na miaka 13, nilipenda kutazama kazi ya maoneysho ya urembo. Nilikuwa nikimfuata dada yangu mkubwa ili kutazama alivyofanya maonyesho ya urembo na nikapenda nilichokiona: wanawake imara, warembo na jasiri wakisherehekea urembo wao wa ndani na nje. Nilipokuwa na miaka 17, nilianza pia maonyesho ya urembo kwa kujifurahisha. Lakini nikatambua haraka kuwa watu hawakushughulika nami. Matajiri walikuwa wabinafsi. Wanamitindo walichukuliwa kama vitu, wala si watu.

Siku moja baada ya rafiki yangu kufokewa tena, nilikuwa na wazo: Ninaweza kufanya kazi nzuri kuliko matajiri hawa! Ninapaswa kumiliki na kuendesha kampuni ya maonyesho ya mtindo ambapo ningalikuwa na uhakika kwamba wanamitindo wanaheshimiwa!

Muda uliposonga nilianza kuamini kabisa wazo langu. Nilitazama kwa karibu namna mambo yalivyokuwa yakifanyika na namna kampuni za maonyesho ya urembo zilivyokuwa zinaendeshwa. Nilijua kuwa nilihitajika kutia bidii ili kulifanikisha hili. Niliwaomba ushauri watu waliokuwa na ujuzi wa biashara. Nilizungumza na vijana wengine na wanamitindo kuhusu ndoto yangu. Kila mtu alinitia moyo!

Wazazi wangu wakaniunga mkono pia. Walisema kila mara kuwa ningetimiza ndoto zangu iwapo ningejaribu kutia bidii zaidi. Nimekuwa nikiwashukuru sana.

Kisha Julai 2011, nilichukua hatua na kuamua kuanzisha biashara yangu binafsi. Kufikia Novemba mwaka huo, nilizindua kampuni yangu binafsi, kwa jina Ikobe Modelling Company!

Huu ulikuwa wakati wa kuvutia lakini wa kutisha. Nikiangalia nyuma, ninajivunia sana kuwa nilikuwa na ujasiri wa kutia bidii na kufuata ndoto zangu. Leo, biashara yangu inaendelea kukua na ninaweza kujisimamia kwa pesa zangu binafsi.

Lakini cha kufurahisha sana ni kwamba nimeweza kuajiri vijana wengine ili waweze kujitegemea pia. Tunafanya kazi pamoja ili kuimarisha uchumi wa Rwanda, na tunaifanya kwa fahari na heshima.

Wasichana, haijalishi ndoto zako ni zipi, kumbuka kila mara kutia bidii, kuwathamini watu wengine, kujiheshimu na kufuata ndoto zako! Ninaamka kila asubuhi nikifahamu kuwa ninafanya kazi ili kuboresha maisha ya baadaye.

Share your feedback