Mambo, naitwa Maria, nina umri wa miaka 20. Nilipokuwa mdogo nilikuwa naishi na shangazi na mjomba wangu. Walinifanya niamini kwamba walikuwa na haki ya kunipiga ama kuninyanyasa kwa sababu tu sikuwa mtoto wao wa kuzaa, na kwamba sikuwa na pakwenda. Kiukweli nilihisi kama nipo kifungoni.
Walikuwa wakinionea sana. Nilipokuwa nikimuomba shangazi aninunulie pedi tuu nilipokuwa kwenye siku zangu, alikuwa ananijibu "tumia hata magazeti" na pale nilipotaka kutengeneza nywele ili nipendeze japo kidogo, alinikuwa ananisema " Enhee kwa hiyo saivi umeanza mambo ya mapenzi eh!? Unataka kujiremba kwa ajili huyo mwanaume wako sio? Kiukweli nilikuwa na hali ngumu sana.
Nilikuwa na maisha magumu sana kipindi hicho. Nilihisi kukatishwa tamaa sana. Yani kupata muda wa kushika vitabu, na kujisomea pamoja na kufanya mazoezi ya shule, ni mpaka pale tu niwe nimemaliza kazi za nyumbani ambazo zilikuwa nyingi mno na ngumu.
Siku moja, baada ya kufikiria kwa muda mrefu, nilijipa ujasiri na nikaamua kuzungumza na mmoja wa walimu wangu ambaye nilikuwa naona namuamini. Hofu ilikuwa imenijaa sana. Kitu kimoja tu kilichonisaidia ni kuwa nilipanga maneno ya kumwambia na niliyafanyia mazoezi kwa kuyaongea kwa sauti, kabla hata ya kwenda kuzungumza na mwalimu. Nafurahi kwamba niliamua kuzungumza nae. Aliyabadili maisha yangu.
Nilipoenda kuongea nae nilimwezea stori ya maisha yangu kama tu nilivyokuwa nimejipanga. Alinitazama machoni halafu akaniambia "hakuna mtu ana haki ya kukupiga ama kukutesa. " Aliambatana na mimi kwenda nyumbani na alikutana na walezi wangu. Aliendelea kuongea nao mara kadhaa katika kuwashawishi. Ilimchukua muda kidogo lakini baadae alinipatia sehemu nyingine ya kuishi mbali na pale nilipokuwa nikiishi mwanzo. Nilipata muda wa kujikita katika masomo yangu na nikaendelea kuwa jasiri.
Nilipokuwa nikiishi na shangazi na mjomba nilikuwa muoga hata kuomba msaada. Lakini nafurahi kwamba niliweza kuomba msaada. Sasa hivi nina furaha na nipo salama na najivunia kwamba nilipata ujasiri wa kuvunja ukimya na imenisaidia kuboresha maisha yangu.
Share your feedback