Dada Milele

Jinsi nilivyopambana na upweke wakati dada yangu alipotoka nyumbani

Kwa miaka mingi dada yangu mkubwa alikuwa rafiki yangu wa dhati. Tulifanya kila kitu pamoja. Tulivaa mavazi yaliyofanana, tulipenda chakula kimoja na aina moja ya filamu. Alinifundisha pia jinsi ya kusoma na kuandika. Wazazi wangu waliweza kumudu kumpeleka shuleni mmoja wetu tu kwa hiyo alinifundisha kila kitu ninachokijua leo. Hata wakati nilipopata hedhi kwa mara ya kwanza, alinifundisha ninachopaswa kufanya. Nilimpenda sana.

Hata hivyo, alipoolewa mambo yalibadilika. Alilazimika kuhamia mji mwingine pamoja na mume wake. Umbali wa saa 7 kutoka kwangu na wazazi wangu. Kwa kuwa sikuenda shuleni alikuwa rafiki yangu wa pekee kwa muda mrefu sana. Sasa alikuwa anahamia mbali na sikuwa na wazo la kutarajia kumwona lini tena.

Alipoondoka nilibaki chumbani mwangu kwa sababu nilihisi sikuwa na mtu mwingine wa kuongea naye. Mama yangu alijaribu kwenda matembezi na mimi lakini sikuwa nahisi kutoka. Siku moja alinisisitizia nimfuate sokoni ili nimsaidie kununua chakula cha nyumbani. Tulipofika kibandani alichukua muda mwingi akiongea na Mama Gloria aliyekuwa akiuza mboga. Niliketi pembeni nikionekana nimechoka hadi msichana aliyeonekana kama ni wa rika langu akaja na kunigusa begani. Alikuwa anaitwa Belinda, binti wa Mama Gloria.

Tukaanza kuongea na nikagundua kwamba tulikuwa na mambo mengi tuliyohusiana . Dada yake mkubwa alitoka nyumbani mwaka uliopita na sasa yeye ndiye mtoto wa pekee nyumbani. Nilipomuuliza jinsi alivyojihisi mpweke alinipa ushauri bora kabisa! Hivi ndivyo alivyosema:

  • Dada yako kutoka nyumbani hakumaanishi alikoma kuwa dada yako. Sisi wote mwishowe tutakua na tuondoke nyumbani. Badala ya kufikiria kuhusu kutokuwepo kwake, jaribu na ukumbuke nyakati zote nzuri mlizoshirikiana pamoja. Nyinyi ni dada milele.
  • Hata wakati unapofikiria uko peke yako kwa hakika hutakuwa peke yako. Kuna wasichana wengine walio katika hali kama yako ambao wanaelewa unavyohisi. Unaweza kuunda mahusiano yenye nguvu kwa kuwasiliana nao.
  • Kujificha dhidi ya kila mtu wakati unapohisi mpweke si jambo nzuri. Marafiki zako wanaweza kukufanya uhisi vizuri kwa hiyo kuwa na watu wenye ucheshi na wakarimu karibu yako. Hata kama huna marafiki kutoka shuleni, tafuta marafiki na wasichana mtaani mwako au katika jamii yako.

Nilisikiliza ushauri wa Belinda na sasa ninajisikia vyema zaidi. Upweke umeisha na nina furaha kupata marafiki wapya!

Share your feedback