Chaguo lako.Maisha yako.
Mambo wasichana wenzangu!
Hakuna jambo gumu kama kuchagua kati ya njia ambayo wazazi wetu wanataka tuifuate na njia tunayotaka wenyewe.
Nawapenda sana wazazi wangu , si unajua damu ni nzito kuliko maji eh!.Lakini hata hivyo bado najua ni muhimu kukumbuka kwamba tumeumbwa tofauti, wenye akili na mioyo tofauti.
Sikuwahi kuwaeleza wazazi wangu kuhusu ndoto yangu ya kuwa mwandishi kwa sababu wenyewe walitaka tu nifanye vizuri katikasomo la hesabu ili baadae nije nifanye kazi kama keshia katika duka la kuuza Rangi hapo mtaani. Walikuwa wakisema makeshia hulipwa vizuri na ni kazi yenye heshima hapa mjini..
Kwa kuwa niliwapenda sana, niliamua kupotezea ndoto zangu na kufuata kile walichokitaka. Niliwaruhusu kufanya maamuzi yote pasipo kuwaingilia.
Ilipokuwa ikifika jioni badala ya kufanya mazoezi ya kujinoa uandishi wangu, nilikuwa nikifanya mazoezi ya hesabu. Shuleni nilitilia mkazo zaidi masomo ya hesabu na biashara badala ya fasihi na uandishi . Hatimaye nilipata kazi kama keshia, nilifurahi kwa sababu wazazi wangu walijivunia sana mtaani kwetu,lakini kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda furaha yangu ilianza kufifia.
Kuzungumzia kuhusu kile unachokitaka sio rahisi lakini inawezekana. Nikiangalia nyuma, najutia kuwa sikusema kile nilichokuwa nakitaka kwa kuongea na wazazi wangu kuhusu uamuzi huo. Ndio, wazazi wapo hapa kwa ajili ya kutusaidia kufanya uamuzi bora lakini wewe pia unahusika vilivyo wanapofanya maamuzi yanayokuhusu.
Wewe elezea tu kile unachokitaka na fuata moyo wako kwa sababu maoni yako ni ya muhimu pia. Usingoje ifike wakati ambapo utaanza kujutia kwa sababu ya mambo ambayo hukuyafanya, ilhali una nafasi ya kuongea nao sasa hivi.
Nimeanza kufuata ndoto zangu kwa kuandika mashairi mafupi. Nitakapokuwa tayari nitawapa wazazi wangu ili wayasome na kuongea nao kuhusu jinsi navyotamani kuwa Mwandishi.
Kumbuka: Usijibebeshe mzigo moyoni kwa kufuata njia "sahihi". Maisha ni safari na sio mashindano. Kwa hiyo hata ukifuata njia fulani kisha ukagundua huipendi, una nafasi ya kugeuka na kufuata njia nyingine. Hujachelewa kufuata ndoto zako.
Share your feedback