Kujifunza namna ya kutumia pesa na kuweka akiba ni siri ya kufanikisha ndoto zako!
Ni vigumu mno kwa rafiki yangu Neema kujibana asitumie hela, anapokuwa nazo mfukoni hasa anapoyaona yale mandazi ya nazi njiani kila anapotoka shule, na mimi pia wakati napoona zile jinzi ninazozipenda zimepunguzwa bei. pamoja na kudhamiria kote kuweka akiba, siku zote huwa ninaishia tu kununua iwe iweje.
Ingawa sio mbaya kujipa raha wakati mwingine,ila ni muhimu pia kuelewa kuwa tamaa zetu za leo kwa vitu vidogo vidogo zinaweza kutukosesha mambo mazuri ya baadae. Haya sasa utajuaje kuwa hiki kitu ni cha muhimu na ni sawa tu kutumia hela kukinunua?
Je Unakihitaji au unataka tu kuwa nacho? Inaweza kuwa kama viatu, vile ni lazima niwe navyo (haswa kama kuna mtoko!) lakini unavihitaji kweli? Mahitaji ni vitu ambavyo huwezi kuishi bila vitu hivyo – chakula cha afya, viatu vya shuleni, dawa ukiwa na mafua. Unavyotaka, ndivyo vilivyo tu! Ni vitu ambavyo ungependa kuwa navyo lakini unaweza kuishi bila hivyo vitu.
Neema husema kuwa fasheni yake inamlipa – mfano hereni anazonunua ni mtaji– yaani anawekeza. Lakini, jamani je ni kweli? Maana hereni za Neema zitaonekana leo nzuri lakini baada miezi michache tu zinakuwa zimeshachakaa. Uwekezaji mzuri ni kwa kitu ambacho kitadumu kwa miaka au kitakufaidisha kwa miezi mingi ijayo. Kwa hiyo badala ya kununua kitu ambacho kinavutia msimu huu ,halafu msimu ujao kinakuwa kimepitwa na fasheni, ni heri Neema aweke hizo pesa kama akiba ili anunue viatu vya shule kwa ajili ya mwaka unaokuja. Si lazima mahitaji yawe ni vitu vikubwa – inaweza kuwa vitu vya kufurahisha nafsi yako – kama pesa za kulipia kozi ya kompyuta hapo mjini.
Aina bora za uwekezaji huwa ni kwa vitu vinavyoweza kuyabadilisha maisha yako – kama cherehani ili uanze kupata pesa zako mwenyewe au twisheni ili kujinoa zaidi. Hivi ni vitu ambavyo huenda ukahitaji kujiwekea akiba. Yaani hiyo inamaanisha hakuna kununua suruali ya jinzi, lakini itakuwa bora kuvumilia, na utajivunia sana wakati ambapo utaweza kutoa pesa ulizotunza na kuitimiza ile ndoto yako!
Share your feedback