Jinamizi la safari ya manunuzi!

Je, Anita anapaswa kusema ukweli kuhusu rafiki yake?

Anita na Sarah walikuwa na umri wa miaka 14 - wamekuwa marafiki tangu utotoni. Siku moja walienda pamoja kununua bidhaa sokoni na kuona viatu vyekundu maridadi vilivyong'aa. Sarah alivipenda viatu hivyo lakini hakuwa na pesa za kutosha za kuvinunua. Kulipokuwa hakuna mtu aliyemuona alivificha haraka mfukoni mwake. Anita alishtuka na alijisikia vibaya sana. Alishangaa kwa nini Sarah alifanya jambo kama hilo.

Kuiba huwa si jambo zuri na kama Sarah alitaka viatu hivyo alipaswa kuhifadhi pesa ili aweze kuvinunua. Sarah alimsihi Anita asimwambie mtu yeyote na wote wakatoka sokoni na kwenda nyumbani.

Anita alipofika nyumbani alionekana amekasirika na mwenye wasiwasi. Alikuwa na wasiwasi sana kuwa huenda kuna mtu alimwona na kwamba anaweza kuwa matatani kwa sababu ya Sarah. Mama yake Anita aligundua kuna jambo baya na akamuuliza ni nini kilichofanyika lakini Anita hakuwa na la kusema. Upande mmoja alikuwa na hofu na alihisi anapaswa kuwa kimya. Upande mwingine alitaka kuwa jasiri na kusema ukweli.

Lakini wanadada, mnafikiri Anita alifanya nini? Alisema ukweli! Kusema uongo kunaweza kuonekana ni kama njia rahisi, lakini hurudi tena na kukusumbua. Huenda kusema ukweli ikawa vigumu lakini ndilo jambo sahihi la kufanya.

Iwapo utawahi kujikuta katika hali kama hii, hapa kuna baadhi ya vidokezo vya kuongea na mtu kuhusiana na hali hiyo:

1. Ongea na mtu mzima unayemwamini
Anita alikuwa sahihi kuongea na mama yake badala ya kuwa na hisia mbaya juu yake. Kabla ya kufunguka, kumbuka kufikiria vyema unachotaka kusema na uwe mtulivu unapokuwa ukijieleza.

2. Kuwa mwaminifu kuhusu hali hiyo.
Kusema ukweli huweza kukuletea imani , na imani kati yako na wazazi wako ni muhimu. Kupata usaidizi wa baadaye ni rahisi pia wakati watu wanapojua wewe ni mtu mwaminifu.

3. Wajibika kwa hatua zako.
Jaribu usishawishiwe na watu wa rika lako, lakini ukifanya kitu kibaya, wajibika kwa hatua zako na uombe msamaha.kutamka neno “pole” kwani husaidia sana.

4. KUWA MKAKAMAVU na JASIRI.
Ukiona kitu kibaya, usiogope kuripoti. Daima fanya jambo la haki. Mwishowe utanufaika. .

Mwishowe mama yake Anita alilazimika kuongea na mama yake Sarah na Sarah alirejesha viatu hivyo na kujifunza somo . Mwanzoni Sarah alikuwa amemkasirikia Anita lakini mwishowe akagundua Anita alikuwa rafiki mzuri.

Share your feedback