Hizi hapa njia 4 za kukabiliana na hali hiyo!
Wavuti hii inahusu wasichana kupigania haki zao. Hii inamaanisha kusaidiana, kutiana moyo na kushirikiana. Lakini tuseme ukweli, sio wakati wote tunajisikia kuwasaidia wenzetu. Wakati mwingine tunaingiwa na wivu na hiyo ni kawaida. Kilicho muhimu ni jinsi unavyokabiliana na wivu na kuugeuza kuwa mwenye kujiamini na mwenye hisia chanya.
Wivu ni hali ya kuwa na kijicho juu ya mafanikio ya mtu mwingine, vitu alivyo navyo au nafasi aliyo nayo. Wivu hutufanya tujihisi hatuko salama na wakati mwingine hutufanya tumtendee mabaya yule mtu tunayemuonea kijicho. Aina hii ya hisia si nzuri kwetu na kwa hiyo tunahitaji kujifunza kuzidhibiti kwa akili.
Ukijiona unaingiwa na wivu kuhusu mtu mwingine, basi hii hapa njia ya kuugeuza ili badala yake ujiamini.
Hakuna haja ya kuyaonea wivu mafanikio ya watu wengine, kwa sababu sisi sote tuna vipaji na talanta za kipekee. Ndani yetu sote mna mbegu za ukuu. Unahitaji tu kujifunza jinsi ya kuzitumia.
Ushindi wa mtu mwingine haumaanishi kwamba wewe umeshindwa. Sisi sote tuna uwezo wetu binafsi. Kwa kuwa tu msichana mmoja amefaulu shuleni kuliko wewe haimaanishi wewe ni wa chini kuliko yeye. Huenda huna uwezo wa kimasomo lakini unaweza kushinda katika mambo mengine kama vile michezo, michezo ya kuigiza na labda ukawa na akili ya biashara. Hebu chunguza uwezo ulio nao, ukijua uwezo wako utakuwa mtu unayejiamini zaidi.
Ukimwona mtu mwingine anafaulu katika kitu ambacho hata wewe ungependa kufaulu, basi ongea naye akuambie kile alichokifanya hadi akafaulu. Badala ya kuona wivu, tumia mafanikio yao kama hamasa ya kukusaidia kufanya bidii zaidi. Watafute wakuhamasishe badala ya kujilinganisha nao kwa njia isiyokuwa nzuri.
Tumia muda kuyatafakari maisha yako na uzidi kuwa mtu bora kuliko mwanzo. Hakuna mtu aliye mkamilifu kwa hiyo kutumia muda wako kukua na kujiboresha ni bora zaidi kuliko kupoteza muda ukitamani maisha yako yangefanana na ya mwingine. Kadiri unavyojijua zaidi ndivyo utakavyojisikia unajiamini zaidi.
Mwisho,kumbuka kuwa "subira yavuta heri". Maendeleo ya pole pole bado ni maendeleo na ushindi wa msichana mmoja haumaanishi wewe umepata hasara. Vivyo hivyo urembo wa msichana mmoja haumaanishi wewe una sura mbaya. Kuna fursa za kumtosha kila mtu!
Share your feedback