Na sijui nifanyeje ili nijisikie poa.
Unajisikia una huzuni na u mpweke? Hauko pekee yako. Ni jambo la kawaida kujisikia hivyo. Unaweza kujisikia una huzuni kutokana na mambo mbalimbali yanayoendelea katika maisha yako, kama vile kutokufaulu katika mitihani au kuwa mbali na mtu unayempenda. Au yawezekana unawaza sana kuhusu mabadiliko ya mwili wako. Unaweza kufanya yafuatayo ili kujisikia sawa.
Mtazamo mzuri: Sio jambo rahisi kuwa na mtazamo mzuri pale unapohisi kutengwa na kila kitu kinachokuzunguka kuonekana mabaya. Lakini unapaswa kujikumbusha vitu vyote vizuri kuhusu wewe. Vitu kama vile jinsi ulivyo mkarimu, jinsi ulivyo jasiri kuanza upya hata pale mambo yanapoharibika, ama chochote tu kizuri kuhusu wewe.
Kuwa na kidaftari cha kuandikia huwa inasaidia pia. Andika vitu vinavyokufanya ujisikie vyema, kama maneno yanayo kuhamasisha kuhusu thamani yako, uimara wako na malengo yako ya maisha. Fanya vitu vidogo vidogo kila siku na utakuwa bora zaidi ndani ya muda mfupi. Kama utakosa kitu cha kuandika basi ongea na wazazi au mlezi wako na uwaulize wakwambie tabia nzuri ulizonazo.
Tafuta fani: Jiunge ama waweza anzisha kikundi. Kukaa karibu na watu wenye tabia kama zako huleta furaha na kukufanya ujisikie vizuri. Labda tuseme wewe unapenda kusoma vitabu, anzisha kikundi cha usomaji vitabu ambapo mtakuwa mnakutana katika maktaba jirani ama shuleni. Lakini pia unaweza jaribu kuunda vikundi vya michezo na utamaduni.
Tenda Mema: Angalia kwenye jamii yako. Je kuna shirika lolote linalohitaji watu wa kujitolea? Au jaribu katika maeneo jirani. Je una jirani mzee anayehitaji mtu wa kumsaidia kwenda sokoni, au mtu anayehitaji mtu wa kumsaidia shughuli za nyumbani? Kabla ya kutenda jambo lolote jema tambua kuwa usalama wako ndio kitu cha kwanza kabisa. Tafuta mtu mzima unayemuamini, kama vile mzazi au mwalimu, ili akusaidie kupata shirika au mtu wa kukusaidia.
Usikae na vitu moyoni: Mueleze mtu mzima unayemuamini kuhusu kile unachijisikia. Kuzungumza vile unavyojisikia ni hatua ya kwanza kabisa ya kupona maumivu ya moyo. Kama hauna mtu mzima unayemuamini, mpigie kiongozi anayetoa msaada kwa watoto au tembelea hospitali.
Ukiwa na msaada sahihi mambo huwa shwari.
Share your feedback