Kuwa rafiki wa dhati na mama yangu

Haikuwa rahisi lakini sasa ni jambo la busara.

Mimi na mama yangu ni watu tofauti kabisa; anapenda msimu wa baridi, ninapenda msimu wa joto, anapendelea chai bila maziwa, napendelea kuongeza maziwa na sukari. Kwa ujumla, huwa hatukubaliani kwa chochote kile.

Hii ilikuwa ikinikatisha tamaa sana. Nilianza kuamini kwamba nisingeweza kuongea naye kuhusu kitu chochote.

Marafiki zangu waliniambia kuhusu wanavyoongea na mama zao kuhusu mambo ambayo sikuweza kumwelezea mama yangu - kama vile mahusiano na shule, nilikuwa nikihisi ni kama hawezi kuelewa.

Hata hivyo nilielewana vizuri na shangazi yangu. Kwa hiyo siku moja nikaongea naye kuhusu uhusiano wangu na mama yangu ulivyo na changamoto. Kwa mshangao wangu, alinielezea kwamba mama yangu alikuwa akihisi hivyo pia; alitaka kuwa karibu na mimi lakini hakuwa na uhakika kuhusu jinsi ya kuwasiliana na mimi na kuzungumza na mimi kuhusu mambo kama vile wavulana na kazi za shuleni.

Shangazi yangu alinishauri nipange siku maalum kwangu na mama yangu ambayo tunaweza kufahamiana. Alinifafanulia kwamba kama ninataka kuwa karibu na mama yangu ninapaswa kufanya hivyo kwa:

  • kuongea naye kwa njia ya kirafiki na ya heshima. Nifikirie ninachotaka kupata kutoka katika mazungumzo hayo na ni hakikishe nimesikiliza maoni yake anapoongea pia.
  • kupanga kuzungumza naye wakati tutakapokuwa sisi peke yetu nyumbani. Kwa njia hiyo ataweza kunipa muda wake bila kutatizwa na wengine.
  • kufanya kitu ambacho wote tunafurahia, kama vile kutazama maonyesho tuyapendayo ya TV au kushughulikia bustani. Hii itasaidia kuondoa vizuizi vyovyote na kufanya mazungumzo kuwa rahisi.

Nikiwa nimeridhika, nilirudi nyumbani na kuanza kutumia ushauri wa shangazi wangu. Nikapanga tarehe nyumbani maongezi yangu mimi na mama yangu. Tulitumia Jumamosi iliyofuata kufahamiana na sasa najisikia vizuri zaidi kuongea na mama yangu kuhusu jambo lolote.

Ninafuraha sana niliomba ushauri wa shangazi yangu siku hiyo kwa sababu mama yangu ndiye mtu nimpendaye sana duniani.

Share your feedback