Kusema kunaweza kukuokoa

Jinsi ya kuanzisha mazungumzo na wazazi wako

"Wazazi wangu hawawezi kunielewa"

Wote tumewahi kuyasema meneno kama haya.

Ukweli ni kwamba tunapaswa kujifunza namna ya kuongea na wazazi na ndugu ambao ni watu wazima ili waweze kutuelewa zaidi. Wote tunafahamu kuzungumza na wazazi kunaweza kuwa jambo la kuogopesha, lakini wao wapo ili kukusaidia na kukuunga mkono unapohitaji msaada. Hivyo sio jambo jema kuwaficha watu wa karibu mambo yako muhimu

Kama hauongei na wazazi wako kila siku, inaweza kuwa vigumu kwako kuanzisha nao mazungumzo. Hivyo anza kuzungumza nao kuhusu mambo madogo madogo. Unaweza kuwauliza kuhusu siku yao ilivyokuwa au hata unaweza kuwaeleza jinsi siku yako ilivyokuwa.

Zifuatazo ni dondoo zitakazo kusaidia kufanya iwe rahisi.

Kuwa na Mpango

Kabla hujaongea na wazazi wako unatakiwa kufanya yafuatayo:

  1. Fikiria juu ya kile unachotaka kusema.
  2. Yaandike mahali, kwa mfano, kama unataka kuomba ruhusa ya kwenda mahali, muda gani unatarajia kurudi, na nani atakuwa kiongozi wako, kama vile mzazi wa rafiki yako au ndugu yako mkubwa, ili kuwafanya wawe huru kukuruhusu.
  3. Chagua unayetaka kuongea nae. Je unataka kuongea na mzazi mmoja au wote wawili? Au unahitaji mzazi mmoja akusaidie kuongea na mzazi mwingine?
  4. Pia unahitajika kuweka muda. Fanya mazungumzo yako wakati wazazi hawapo bize ili waweze kukusikiliza.

Kuwa Jasiri

Usiruhusu uoga ukuzuie kuzungumza na wazazi wako. Haijalishi mada mnayotaka kuizungumza, kuongea ni jambo jema.

Kuwa Muwazi na nenda moja kwa moja kwenye ponti

Wakati unaongea na wazazi wako unatakiwa kuwa mtulivu ili waweza kukuelewa kirahisi. Usifanye mambo kuwa makubwa sana. Kuwa mkweli. Fanya yawe mazungumzo rahisi na mepesi. Wafanye wajue kile unachokifikiria, unachojisikia na unachokitaka. Ni muhimu sana wazazi wako kuelewa kila unachokisema.

Sikiliza

Jambo muhimu sana katika mawasiliano ni uwezo wa kukaa kimya na kusikiliza. Hakikisha unaelewa kile ambacho wazazi wako wanakuambia ili uweze kuwajibu vizuri. Kama haukubaliani na kile wanachokisema, kuwa kama mtu mzima na zungumza nao kwa sauti ya adabu na yenye mawazo chanya. Hii itawafanya wachukulie kwa uzito kile unachokisema.

Share your feedback