Kuendelea kusonga mbele baada ya wazazi wangu kutengana

Niligundua ilikuwa inatuumiza sote.

Miaka michache iliyopita, mambo yalikuwa magumu sana nyumbani. Wazazi wangu walikuwa wakipigana sana na mwisho wa siku walitengana, na baba yangu akaamua akaondoka. Ilikuwa ni vigumu kwetu sisi sote, hasa mama yangu. Ilimpasa yeye peke yake kunitunza mimi na wadogo zangu wawili, huku akiwa anaendelea kufanya kazi.

Ilibidi sisi sote tuzoee maisha ya bila baba .Nikiwa kama mkubwa wao, nilisikia kuwajibika kumsaidia mama yangu pale nilipoweza, lakini nilichoishia kufanya ni kugombana naye tu na machozi mengi ya kutosha nikiwaza juu ya yale tunayoyapitia. Hii wala haikusaidia chochote. Nilianza kutambua kwamba kununa kusingetatua chochote na kwamba sio mimi tu niliyekuwa naumia katika kujaribu kukubaliana na hali halisi.

Hivyo nilibadilisha mtazamo wangu. Siku moja mchana niliamua kumsaidia mdogo wangu kazi yake aliyopewa shuleni,huku nikiendelea na ya kwangu. Alijisikia vizuri kukaa pembeni yangu na nilijisikia vizuri kuona kwamba mama yangu hatokuwa na kibarua cha kumsaidia tena mdogo wangu kazi zake za shule anapokuwa katoka kazi,Kwa hiyo hii niliifanya kama ratiba na mama yangu alinishukuru sana. Pia niliamua kuwa namsaidia mama jikoni wakati wa kupika msosi – yaani kuandaa meza, ku katakata mboga na kuosha vyombo. Hata niliweza kumuomba shangazi yetu anifundishe baadhi ya mapishi rahisi rahisi ambayo ningeweza kuyapika ili mama nae apate muda wa kupumzika.Alikuwa akifurahia sana kila mara alipokuwa akiingia mlangoni! na kukuta chakula mezani nilichokuwa nimeandaa.

Mambo yamekuwa mazuri kiasi nyumbani – na uzuri ni kwamba mimi na mama yangu tuna urafiki wa karibu zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzo. Bado huwa kuna kubishana kwa hapa na pale, lakini kwa pamoja tumesaidiana ili tuweze kuvuka katika hiki kipindi kigumu. Hata itokee nini,sisi tutabaki kuwa wamoja daima.

Nimejifunza kuwa familia ni kitu muhimu sana, na ikiwa sote tutakuwa na mtazamo chanya na kufanya kazi pamoja, tunaweza kuvuka majaribu yoyote yale.

Share your feedback