Hatua 4 zitakazo kusaidia kutimiza malengo yako
Huwa naupenda mno mwanzo wa mwaka. Kila januari, huwa napata hisia na kuamini "kila kitu kinawezekana" na huwa najawa na shauku na nguvu ya kufanya vitu vipya vinavyonifurahisha. Ila niseme tu ukweli, nimeanza kujisikia hivi kuanzia mwaka jana tu pale ambapo mwalimu wetu wa sayansi, aitwaye Massawe, alipotufundisha jinsi ya kuwa na mwaka bora kabisa.
Tulipokuwa katika muhula mpya wa kwanza, mwalimu Massawe alituagiza tuandike malengo yetu makubwa matatu ambayo tulihitaji kuyatimiza katika mwaka ule. Nikawaza "nataka kumjengea mama yangu nyumba, nataka kuwa na gari na kujiendesha mwenyewe, natamani kusafiri kwenda nchi zingine kufurahia maisha, nilijisemea siwezi kuyatimiza yote haya ndani ya mwaka mmoja. Hivyo niliamua kuomba msaada kutoka kwa mwalimu Massawe. Aliniambia napaswa kufikiria kitu ambacho ningekifanya kwa sasa ambacho kingenisaidia kuyatimiza malengo yangu makubwa niliyokuwa nayo. Nikawaza, "sayansi ndilo somo nililokuwa nalipenda sana, labda siku moja ninaweza kuwa mwanasayansi na kujipatia kipato nilichokihitaji ili kununua nyumba, gari na kusafiri" hivyo kitu pekee ambacho ningeweza kukifanya kwa sasa ni kujiunga na klabu ya sayansi na nijaribu kwa kila hali kushinda mashindano ya sayansi kimkoa. Rafiki yangu Amina naye aliamua kujiunga na klabu ya sayansi pamoja na mimi. Tulifanya mazoezi mengi jioni baada ya shule na kila mwisho wa wiki tulikuwa tunakutana ili kujipima. Mimi na yeye ndio tulikuwa wasichana pekee katika klabu yetu, wavulana walituona kama hatukuwa na akili kama wao. Na muda sio mrefu tulianza kujibu maswali kwa haraka zaidi kuliko wao na baadhi yao walianza kutuheshimu!
Klabu yetu ilifuzu kwenda kushiriki mashindano ya sayansi ngazi ya mkoa na tulishika nafasi ya 3 Kati ya timu 10 zilizoshiriki. Hii ilinifanya nione naweza kufanya kitu chochote kile kama nitajituma na kujiamini. Hakuna ndoto ninayoiona kubwa na isiyoweza kutimizwa tena, mwaka huu, naamini nitapata nafasi ya kushiriki katika mashindano ya kitaifa.
Share your feedback
Mawazo yako
Oyavp
Machi 20, 2022, 8:25 p.m
Latest Reply
Naombaurafik