Kuwa mwenye furaha na uliyeridhika.
Je unafikiria kuhusu kuwa na mpenzi? yaani Waala hauko peke yako. Kuwa na mpenzi ni kitu cha kawaida kama sehemu ya ukuaji. Na linaweza kuwa jambo la kufurahisha pia.
Baada ya kusema hayo, ni vyema uwe na mahusiano sahihi na salama. Yale ambayo yatakuletea furaha, uhuru na kujihisi umekamilika. Uhusiano ambao utakuruhusu kuwa huru zaidi. Dondoo hizi zitakusaidia kujua mahali pa kuanzia.
Kuweni marafiki
Mahusiano mazuri ya kimapenzi huanza na urafiki. Mahusiano mazuri hujengwa na uaminifu, usawa, na heshima kwa wote. Mnapoanza mahusiano kama marafiki, vitu hivi huonekana kwa urahisi.
Ni vyema mkafahamiana vizuri kabla hamjapiga hatua kubwa zaidi. Itakuwa rahisi kujua kama mnapenda vitu vinavyofanana, mna mitazamo sawa, au maadili sawa nk. Na pia utaweza kujua kama kweli huyu mtu ni mtu sahihi atakayekubali madhaifu yako na kukuchukulia kama jinsi ulivyo.
Zungumza
Unapokuwa katika mahusiano na mtu unapaswa kujisikia huru kuzungumza nae. Kama kuna kitu kinakuudhi ni vyema kukizungumza kuliko kukiweka moyoni. Kwa mfano, kama mpenzi wako anakulazimisha kujamiiana na haupo tayari unapaswa kumueleza vile unavyojisikia. Maana mpenzi wako hawezi kusoma mawazo yako hivyo. Kuwa muwazi, na mkweli kwa kadri uwezavyo.
Usifanywe kuwa mpenzi wa siri na yeyote
Moja ya kitu kizuri sana katika mahusiano ni kutambulishwa kwa marafiki wa mpenzi wako sio?. Kama wewe binafsi huwezi kuwaambia marafiki zako wa karibu kuhusu mpenzi wako, hii inamaanisha kuna jambo halipo sawa. Hii pia ni sawa na pale ambapo mpenzi wako anataka mkutane katika maeneo ya siri ambapo hakuna atakayeweza kuwaona mkiwa pamoja, unapaswa tu kujiuliza Je haya ni mapenzi ya dhati kweli? kama anaogopa au anasikia aibu kuonekana na wewe mbele za watu? Inabidi utafakari sana.
Kila mmoja wenu anapaswa apate muda wa kukutana na marafiki wa mpenzi wake,Hii Itawafanya mfahamu kile mnachokifanya.
Jipe muda wako binafsi
Kuwa katika mahusiano haimaanishi mgandane kama kupe. Mnahitaji kupeana nafasi bwana. Hampaswi kuwapoteza marafiki zenu eti kisa mpo katika mahusiano. Au hata kuacha kufanya vitu ulivokuwa ukivipenda. Mara moja moja jipe nafasi ya kufanya mambo yako binafsi. Kuna furaha katika kufanya vitu unavyovipenda.
Kuwa mkarimu na mwenye kusaidia
Sio vizuri kuitana majina ya kuvunjiana heshima au kununiana. hamtakiwi kugombezana au kupigana - haijalishi umekasirika kiasi gani. Daima tianeni moyo badala ya kukatishana tamaa. Amini ndoto za kila mmoja na mhamasishane kuzitimiza. Ni kweli, mtatofautiana wakati mwingine. Lakini mambo yanaweza kusuluhishwa kwa mbinu sahihi na za kiutu mzima.
Kumbuka, unapaswa kujisikia uko salama, unapendwa na unakubalika. Una haki ya kuvunja mahusiano ambayo unaohisi hauna furaha nayo na sio salama. Kama una tatizo kuhusu mahusiano yako, zungumza na mtu mzima unayemwamini mara moja.
Share your feedback