Hawana tofauti!
Naitwa Anna; nina miaka 16. Ni mtoto wa kwanza katika familia yetu na nina wadogo wawili mapacha Jenny na Jimmy wana miaka 12.
Katika umri wa miaka 12, Jenny alianza kubadilika kimaumbile haraka na kuonekana mkubwa kuliko pacha wake Jimmy. Mabadiliko hayo yalimfanya Jenny ajisikie tofauti kwenye mwili wake. Alikuja kueleza tatizo lake kwangu. Nilimwambia kuwa yuko katika kipindi cha Balehe. Na kila mtu darasani kwake atapitia hicho kipindi. Wasichana watabadilika kuwa wanawake na wavulana watabadilika kuwa wanaume. Jenny alibisha sababu Jimmy hakuwa anabadilika. Nilimwambia Jimmy atabadilika pia, ila mara nyingi wasichana wanawahi kubalehe kuliko wavulana.
Siku moja jirani yetu Benny alikuja kucheza na Jenny na Jimmy. Benny aliwaambia Jenny na Jimmy kuwa anabadilika kuwa mwanaume hivyo anataka aanze kufanya mambo ya kikubwa. Niliona mdogo wangu amefurahi sana kuona Benny anapitia mabadiliko kama yeye. Kwa pamoja walijadiliana mabadiliko ya ndani na nje ya miili yao.
Waligundua kuna mabadiliko wanayoyapata kwa pamoja kama; kurefuka na kuongezeka uzitoi. Pia waligundua kuwa wasichana na wavulana wanapata mabadiliko mengine tofauti kabisa. Jenny anapata hedhi kila mwezi na Jimmy anapata ndoto nyevu siku zingine akilala.
Walikuwa na maswali ya kuniuliza mimi kama dada mkubwa. Walitaka kujua kama wanabidi wabadili tabia sababu wanabalehe. Niliwaambia hamna haja ya kubadili tabia waendelee kuwa wenyewe na kufurahia mabadiliko.
Nimefurahi sana kuona Jenny aliweza kuongea na mimi kuhusu mabadiliko ya mwili wake. Kwani niliweza kumsaidia kujiandaa kwa mabadiliko mengi zaidi yanayokuja, ili kumfanya afurahie kipindi chake cha balehe na kumpa taarifa sahihi kuhusu mwili wake. Na sasa anamsaidia Jimmy kujiandaa na mabadiliko ya mwili.
Ni kitu cha kawaida kabisa, kuongelea mabadiliko ya mwili wako na rafiki zako, mzazi au mtu aliyepitia kipindi cha balehe. Ilimradi tu unajisikia huru kuongea naye. Nakupa dondoo za kukusaidia kujadili; hakikisha mazungumzo yana utulivu, elezea swali lako kwa ufasaha, sikiliza kwa makini ushauri unaopewa.
Share your feedback