Nywele za mwilini ni kitu cha kawaida na hututokea sote
Mpendwa Dada Mkubwa,
Nimeanza kuona nywele kwenye mwili wangu sehemu ambazo zamani hazikuwa na nywele kabisaa.Je nifanyeje?
Naomba Msaada.
Amina
Mpendwa Amina
Ahsante kwa swali lako. Kwanza kabisa ni kawaida kwa nywele kuanza kuota katika sehemu mbalimbali mwilini,kama kwenye makwapa au sehemu za siri, tunapoanza kubalehe. Najua inaweza kuwa kitu cha kushangaza sana na cha aibu., lakini ni kitu kinachomtokea kila mtu.Najua Inaleta maswali mengi kushuhudia miili yetu ikibadilika na wasichana wengi wana maswali mengi kuhusu mabadiliko haya.
Nywele zinazoota sehemu za siri tunaziita Mavuzi na ni sehemu ya maisha. Inatokea kwa wavulana na wasichana kadri tunapokuwa wakubwa, na ni kawaida kama nywele zinazokua kwenye kichwa chako. Wasichana wengi huanza kuota nywele kabla ya kuanza hedhi zao. Inaweza kuanza kama nyembamba na nyepesi lakini kwa kawaida huwa nyeusi zaidi na nzito kadri muda unavyozidi kwenda. Watu wengine wanapendelea kuzinyoa nywele zao zote, na wengine hupenda kuzipunguza. Ni uchaguzi wako tu kibinafsi na hakuna njia sahihi au isiyo sahihi. Hakuna mtu anayepaswa kukuhimiza kutoa nywele zako, kwa sababu ni mwili wako, na hiyo inamaanisha ni uchaguzi wako.
Mavuzi ni afya. Inasaidia kuzuia bakteria hatari kuingia katika uke na kulinda midomo ya uke dhidi ya msuguano na usumbufu utokanao na chupi yako.
Nywele za mwili ni sehemu ya asili ya maisha na sio kitu cha kuonea aibu. Ni moja ya mabadiliko mengi tunayopitia wakati wa kubalehe. Wakati wowote unapohisi kuchanganyikiwa au kujisikia una hofu, daima wasiliana na rafiki au mtu wa familia anayeaminika na kumbuka hauko pekee yako.
Nawapenda
Dada Mkubwa
Share your feedback