Homoni! Ni kitu gani?

Jinsi ya kuzichukulia poa homoni!

Je, unapatwa na zile siku ambazo unashindwa kabisa kuzuia mabadiliko ya hisia zako? Je, umeona nywele zikitokeza kwenye maeneo mapya ya mwili? Au kuamka na ukajisikia kama umeongezeka inchi kadhaa ulipokuwa usingizini? Au labda mvulana fulani ulokuwa unamuona mkorofi darasani ameanza kukuvutia kidogo hivi – basi, umekisia vema, Ndio homoni zako shosti zipo kazini.

Homoni ni kemikali maalum zilizo katika mwili wako ambazo huanza kubadilika wakati wa kubalehe.

Kwa wasichana wakati unapovunja ungo, ovari zako huanza kutoa homoni zinazoitwa estrojeni, projesteroni na testosteroni. Wakati mwili wako unapoanza kutoa homoni hizi, matiti yako huanza kukua, mwili wako utaanza kupata umbo fulani la ukweli! na hedhi yako itaanza.

Kwa wavulana, viwango vya testosteroni huongezeka – ndiyo sababu unaweza kusikia sauti yao inakuwa ya "bezi" kuota ndevu na miili yao inakuwa mikubwa na mipana.

Hii inaweza kuwapa maswali mengi sana wasichana na wavulana kuelewa mabadiliko mengi ya kimwili na ya kihisia kwenye mwili wao wakati homoni zinapoanza kutokea. Nilipoanza kubalehe, niliongezeka uzito, matiti yangu yalikua haraka sana kuliko ya marafiki zangu, na nilianza kujiuliza – “Je, hii ni kawaida?!”

Sikujua nizungumze na nani kuhusu hili. Nilikuwa nasikia aibu sana kuwauliza wazazi wangu, na mimi ndo dada mkubwa pale nyumbani.Kwa bahati nzuri, Daktari wa shule yetu alikuwa ni mzuri sana, na aliweza kunisaidia na maswali yoyote niliyokuwa nayo. mfano kama “Kwa nini huwa ninakuwa na huzuni na hasira pia kabla ya hedhi yangu?” au “Kwanini huwa nina hamu ya kula sukari sana wakati wa hedhi yangu?” Daktari alinifundisha kwamba miili yetu hutofautiana na hukaribia kubalehe katika hatua tofauti – lakini mabadiliko haya yote ni ya kawaida. , Badala ya kusikiliza dhana potofu nilizowahi kuzisikia alinisaidia katika kunifundisha ukweli kuhusu homoni.

Jambo kubwa nililojifunza ni kwamba, kama hedhi yetu ilivyo, homoni zetu pia hupitia mzunguko – hivyo ni muhimu kujifunza kukubaliana na jinzi hisia zetu zinavyobadilika kila mwezi.

Share your feedback