Fuata hatua hizi 3
Mambo vipi msichana!
Mkumbo rika ni changamoto kwelikweli. Je umewahi kuwa katika hali ya kutokuwa tayari kufanya jambo lakini ukalifanya kwa sababu tu wengine wanalifanya? Je wajua kwamba wote tumewahi kuwa katika Hali hiyo? Sio jambo rahisi kujifunza kusema HAPANA lakini unaweza kujifunza na kujenga tabia ya kusema hapana.
Hatua ya 1 - Epuka kujiweka katika mazingira magumu.
Tuchukulie haupo tayari kujamiana lakini mpenzi wako anakualika kwenda nyumbani kwake kupiga stori masaa ya usiku. Unajua kabisa anatamani kufanya ngono na wewe japo wewe haupo tayari kufanya hivyo. Je utafanya nini?
A. Kwenda tu nyumbani kwake Masaa ya usiku.
B. kusema HAPANA na kumuomba mkutane katika maeneo yenye watu wengi.
Jibu sahihi ni chaguo B! Kama unaweza kuepuka kuwa katika mazingira hatarishi basi fanya hivyo. "Si unajua majuto ni mjukuu" hivyo kama tunaweza kuyaepuka kwa kufanya maamuzi sahihi hii ni hatua moja nzuri ya kukuweka kuwa salama. Usikae na watu wanaokufanya ujisikie vibaya ama kukusukuma kufanya vitu ambavyo haupo tayari kuvifanya.
Hatua ya 2 - Fikiria madhara yatokanayo na maamuzi yako.
Kila unapotaka kusema NDIYO au HAPANA kuhusu uamuzi wowote ule usifanye hivyo kwa kufuata hisia zako. Chukua muda kutafakari vizuri na jiulize nini kitakuwa matokeo ya uamuzi wako. Kama unafurahishwa na matokeo basi ni jambo jema. Lakini kama haujisikii vizuri jinsi mambo yatakavyokuwa basi kuwa jasiri na mwelevu kusema HAPANA na kuondoka.
Kwa mfano kuna athari nyingi zitokanazo na kufanya ngono katika umri mdogo kama vile Majuto, hofu na kuchanganyikiwa. Lakini pia unaweza kupata ujauzito kama hautotumia Kinga. Hivyo kama haupo tayari kukabiliana na haya njia sahihi sana ni kusema HAPANA.
Hatua ya 3 - Zungumza na Jitetee
Sauti yako ni ya muhimu. Mawazo yako ni muhimu. Usimruhusu mtu mwingine kukuambia tofauti. Tambua unayo nguvu ya kuamua jinsi unavyotaka maisha yako yawe. Hivyo kuwa mkweli kwa nafsi yako.
Hebu tuchukulie ulichagua chaguo A, na ukaenda nyumbani kwa mpenzi wako usiku ule. Na akakuomba mfanye ngono na haupo tayari kufanya hivyo, Una haki ya kusema HAPANA.
Ni mwili wako hivyo unawezo wa kuamua. Kisa tu umeenda nyumbani kwake haimpi haki ya kufanya ngono na wewe.
Simamia kile unachokiamini ni cha muhimu. Usikae kimya pale unapoona kitu hakipo sawa.
Inaweza kuwa vigumu kusema HAPANA, ila ni muhimu kusimamia kile unachokiamini na unachojisikia ni kitu sawa.
Share your feedback