Jinsi nilivyomwambia baba kuhusu hedhi yangu!

Haikuwa mbaya kama nilivyofikiria

Nilipovunja Ungo,sikushtuka wala kuogopa kwa sababu kwenye kundi la mashosti zangu tulishawahi kuongelea sana kuhusu hedhi na mmoja au wawili kati yetu tayari walikuwa wameshapata za kwao miezi michache iliopita.

Kilichokua kinaniogopesha hasa ni namna ya kumwambia Baba yangu.

Nyumbani, yupo baba yangu, mimi na dada yangu mdogo tu. Wakati mwingine ni vigumu kueleza kwake “mambo ya wasichana” kwa sababu hajapitia mambo haya. Lakini kwa hili, nilijua ilibidi tuliongelee tu.

Kabla ya kuongea nae niliandika namna ningekuja kumuelezea.Natambua anajua hedhi ilivyo lakini nilitaka atambue kuwa hili ni tukio muhimu sana katika maisha yangu ,na kwa vile mama hayupo nasi tena nahitaji msaada wake kwa ajili ya kununua pedi,na pengine dawa za maumivu endapo nitakuwa na maumivu ya tumbo au kichwa.

Siku moja baada ya chakula cha usiku mdogo wangu wa kike akiwa ameshaenda kulala,nilipiga moyo konde na kumwomba baba kama tungeweza kuongea.Moyo wangu ulikua unadunda kwa kasi,lakini baada ya kumueleza uso wake ulionesha wazi kuwa alikuwa tayari kunisaidia.Alinisifia kwa ujasiri wangu kuweza kumuambia kitu kama hicho na akanihakikishia tu kwamba yeyé yupo kwa ajili yangu wakati wowote nikiwa na maswali au kuhitaji chochote na kwamba nisione aibu kumwambia chochote.

Nilijisikia mwepesi kushusha huo mzigo,hatua hii katika maisha yangu ingekuwa ngumu sana lakini baba yangu alilichukulia poa sana swala hili,na kwa vile sasa amenihakikishia sapoti yake najisikia poa sana.

Kwa hiyo unapohitaji kubonga na mzazi au mlezi kuhusi mambo hedhi au mada nyingine nyeti ambayo unaona aibu au wasiwasi kumshirikisha,jaribu vidokezo hivi:

  1. Jiamini (hata kama unahisi huna ujasiri ndani yako!).
  2. Uwe mtolivu na usiwe na aibu – hedhi ni jambo la kawaida na lisilopingika katika maisha ya binadamu.
  3. Omba msaada pale unapohitaji.
  4. Eleza hisia zako kwa uwazi.

Unaweza!

Share your feedback