Kubalehe kumenipata mapema
Unapokuwa mtoto unakuwa na hamu sana ya kuwa mkubwa. Nakumbuka nilikuwa na mazoea ya kuwa karibu sana na dada yangu na marafiki zake pia. Nilikuwa nachukia nikiambiwa na watu ya kuwa mimi bado mtoto sana. Sikuwa najisikia kabisa ya kuwa eti mi ni mdogo – Yaani nilikuwa najiona mimi ni Mdada!
Ila Nadhani nilianza kuongea mapema sana , maana kukua si rahisi kama inavyoonekana. Huwa inakuja na hatua muhimu ya Kubalehe katika maisha. Ubalehe ni wakati miili yetu inaanza kupitia mabadiliko kadhaa kama matiti kukua na makalio kuwa makubwa,vinyweleo kuota mikononi na miguuni. Ni wakati ambao homoni zetu za ukuaji zinapoanza kufanya kazi. Kwa kawaidia hali hii huanza katika umri kati ya miaka 8-13, lakini kwa upande wangu ilianza mapema.
Niligundua tofauti hii wakati watoto wengine niliokuwa nao walivyoanza kuwa wakiongelea kuhusu mwili wangu. wakati mwingine walikuwa wananiboa eti wanasema, “Una vinyweleo kama mwanaume.” Au “Mbona una matiti makubwa sana – au una mimba?”
Kuwa wa kwanza kubalehe kulinifanya nijihisi kama niliyetoka sayari nyingine. Nilikuwa sipendi jinsi walivyokuwa wananisema, hivyo nika amua kumwambia mama yangu maana ni mtu ninayemuamini sana.
Mama alinifariji sana. Aliniambia niwapotezee tuu , Kwa vile hawakuelewa kwa nini nilikuwa nikionekana tofauti, ilikuwa rahisi kunionea, lakini hawajui kuwa kumbe ningeweza kuwasaidia kwa kuwafundisha. Pia alinifundisha kuwa kubalehe ni sehemu msingi katika ukuuaji wa mtu na sipaswi kuona aibu kufikia hatua hiyo mapema zaidi kuliko watu wengine.Mmmh Ndio, inaweza kuwa hali ya kujisikia aibu hivi kidogo, lakini kwa ujumla ni wakati wa mabadiliko poa tuu. Hakuna mtu yeyote aliye na haki ya kukutania kuhusu mwili wako.
Nikiangalia nyuma wakati yote hayo yakitendeka, niligundua kwamba wazo la kuzungumza na mama lilikua bora sana.Kuongea nae kuhusu mabadiliko niliyokuwa nayapitia kulinifanya nijisikie kujiamini na kutokuona aibu.Kwa kuvunja ungo mapema imeniwezesha pia kuwaongoza wasichana wengine.
Hakika inaonesha hakuna baya lisilokuwa na faida kwa upande mwingine.
Kama wewe ni Msichana kama mimi ambaye umevunja ungo mapema hakikisha hufichi hisia zako kuhusu jambo hilo,tafuta mtu unaemwamini na ufunguke.Anaweza kukusaidia kubadili mtazamo wako na kujisikia bora zaidi.
Usipitie haya peke yako!
Share your feedback