Mgeni Hedhi kaja bila hodi!

Jinsi nilivyoikabili hali hii.

Siku moja nilipokuwa shuleni niliinuka kutoka kwenye kiti kumbe sketi yangu ilikuwa imechafuka mno na damu maana nilianza hedhi bila kujijua. Nilikaa chini haraka kwani nilisikia kuchanganyikiwa na sikujua chakufanya.

Huwezi ukajua siku utakayovunja ungo maana huja bila kutarajiwa, kwangu ilinitokea nikiwa katika kipindi cha hesabu cha mwl Monica.

Nilimuandikia kikaratasi rafiki yangu kipenzi Amina, alikuwa amekaa kiti cha tatu kutoka kwangu. Tulisubiri kipindi kilipoisha alinisaidia kwenda kumwambia mwl Monica na wakanisaidia kwenda chooni na kujisafisha na mwl Monica alinisaidia kupata sketi nyinyine ya kuvaa.

Nilimpigia mama simu na kumueleza kilichonipata. Moyoni nilijisikia uoga japo tulikuwa tumekwisha liongelea hapo awali. Alifurahi sana na akaniambia ‘’hongera mwanangu’’.Wakati namsimulia kilichotoea alikuwa karibu na dada yangu naye alifurahi kusikia nimevunja ungo. Hili lilinipa ujasiri kiasi kwani nilijua watanisadia namna ya kukabiliana na hedhi yangu.

Tuliporudi nyumbani kutoka shule amina alikuja na wasichana wengine nyumbani na walinieleza uzoefu wao kuhusu hedhi huku tukila mahindi ya kuchoma ambayo mama aliniletea alipotoka kazini.

Stori ta Sara ndiyo ilinishtua kidogo. Alivunja ungo akiwa darasa la nne.

Lakini mwalimu aliyekuwa akiwafundisha aligundua mapema na akawatoa wanafunzi wengi haraka bila kutokea tatizo lolote.

Wiki chache zilizopita, Halima alishtuka wakati pedi ilipoanguka kutoka kwenye begi lake, halafu ni mbele ya ‘boifrendi’ wake Tom. Lakini Tom alichukua ile pedi , akampa na akatabasamu tu. Kisha wakaenda kwenye darasa lingine pamoja na hakukuwa hata na ishu kubwa.

Baada ya kubadilishana stori za hedhi, nilihisi kuwa jasiri zaidi kukubali hali hii mpya katika maisha yangu. Sitaacha kwenda shule, kucheza au kwenda bichi na na wenzangu kwa sababu ya hofu yoyote kuhusu hedhi yangu. Hakuna kitu cha kunifanya kuona aibu! Hata nikikwama katika hali mbaya – marafiki zangu, walimu na wazazi wapo kwa ajili ya kunisaidia.

Share your feedback