Mungu wangu!
Ninaitwa Aisha nina miaka 16, ninaishi Msasani, Dar es Salaam, Tanzania, ninaishi na baba yangu na kaka yangu. Mama yangu alifariki nikiwa mdogo.
Nilipokuwa na miaka 11, niliona damu kwenye nguo yangu ya ndani. Nilichanganyikiwa. Sikujua imetoka wapi. Nilitumia matambara kujisitiri.
Baadae nilijua toka kwa rafiki zangu kuwa nimepata hedhi. Nilikuwa na maswali mengi ila sikujua wa kumwuliza.
Nilisoma stori inayoelezea "Jinsi ya kuongea na baba yako kuhusu hedhi" Nikapata ujasiri wa kuongea na baba. Mara ya kwanza Baba hakutaka kuongea na mimi, alidai mimi bado mdogo. Nilimwambia nimeshapata hedhi na nataka kujua zaidi. Baba alinielewa na kunielezea; watoto wakike wanazaliwa na mayai zaidi ya elfu yanayoitwa ovari, mshipa wa falopio, na tumbo la uzazi kitaalamu uterasi. Mishipa ya uterasi ni mikubwa inaweza kubeba mtoto tumboni. Msichana anapofikia umri wa kubalehe, kila mwezi yai linachomoka na kupita kwenye mishipa ya falopio kwenda kwenye tumbo la uzazi. Yai hilo lisipokutana na mbegu ya mwanaume baada ya siku moja linaharibika; hapo ngozi nyembamba ya tumbo la uzazi, iliyotanuka kwa damu ili kupokea na kulisha mimba, inachanikachanika, nakutoka pamoja na yai kama damu,hiyo ndiyo inaitwa hedhi.
Mzunguko wa hedhi unatokea kila mwezi kwa miaka mingi, kasoro tu kipindi ambacho mwanamke ni mjamzito, anamatatizo ya lishe au msongo wa mawazo.
Miezi michache baadaye, mwalimu alitufundisha somo la hedhi darasani. Wavulana walitaka kujua zaidi. Niliwaeleza kwa furaha na ujasiri. Walielewa somo vizuri. Baadhi ya wasichana walikuwa wanaona aibu, niliwaambia hedhi siyo kitu cha kuogopa au kuona aibu kuongelea- ni jambo la kawaida na ishara ya kuwa unaelekea kuwa mwanamke.
Niambie umeshapata hedhi? Siku yako ya kwanza ilikuwaje?
Share your feedback