Maumivu ya kila mara wakati wa Hedhi?

Njia za kukusaidia kujisikia nafuu hata wakati hali inapozidi kuwa mbaya.

Kubalehe, Chunusi, Hedhi…… Haya ni mambo mengi mapya ya kukabiliana nayo!

Safari ya kuwa mwanamke ina raha na changamoto zake.Tuko hapa kukusaidia

Tunatambua kuwa maumivu ya wakati ukiwa kwenye siku zako yanaweza kuwa makali sana. Unasikia maumivu ya mwili, unajisikia uchovu zaidi ya kawaida, na ndani ya mwili unajisikia kama umepigwa yaani najisikia hovyo tu. Na mbaya zaidi hali hii inatokea kila mwezi.

Nini msichana anatakiwa kufanya? Je uruhusu kuteseka? Au unywe dawa ili kusaidia kuondoa maumivu? Hapana! Zifuatazo ni mbinu za asili zitakazokusaidia kujisikia vizuri na mwenye afya katika kipindi kama hiki cha kila mwezi.

Kula lishe bora

Matunda na mboga mboga ni njia nzuri sana ya kukabiliana na hamu ya kula vitu vya sukari na njaa za hapa na pale. Jambo zuri zaidi ni kwamba vyakula hivi ni vizuri kwa afya yako. Vimejaa vitamini za kutosha na nyuzi nyuzi ambazo mwili huitaji ili kuwa imara na mwenye nguvu.Lakini pia vyakula hivi vitakupa nguvu kuliko ulaji wa chocolate na vitakusaidia kuepuka kupata chunusi zitokanazo na ulaji wa vyakula vya sukari. Jambo zuri zaidi ni kwamba upatikanaji wa matunda na mboga mboga ni rahisi. Inawezekana jikoni kwenu kuna kapu limejaa vitu hivi, hivi.

Jitahidi ukiwa msafi

Tunapokuwa kwenye hedhi, tezi zetu za jasho na zile zinazotoa mafuta huwa zinafanya kazi mara mbili zaidi katika kipindi hiki. Kuoga maji ya moto au kuoga mara kwa mara kutakusaidia kuondoa jasho na mafuta kwenye ngozi na kuzifanya neva zako kujisikia vizuri na hata kukupunguzia maumivu. Hakikisha unanawa uso wako kabla hujaenda kulala, uso wenye mafuta mengi husababisha chunusi.

Unapokuwa kwenye hedhi, sehemu zako za siri huwa zinakuwa rahisi kupata maambukizi hivyo unyevu unyevu ukizidi unaweza kufanya kupata maambukizi ya bakteria na kuvu (fungus). Ili kuepuka kupata miwasho, safisha eneo hili vizuri (safisha eneo la nje pekee - na sio ndani) kwa kutumia maji safi na sabuni ya kawaida na kisha jikaushe vizuri na taulo Safi.Unaweza kuwa umesikia kuwa kutumia sabuni katika kuosha sehemu za siri ni mbaya lakini hii si kweli kama utahakikisha unatumia kusafisha eneo la nje tu na kujikausha vizuri.

Enhee! hebu tuambie Binti,kuna lolote umewahi sikia labda kuhusu hedhi? tuandikie hapo chini kwenye sehemu ya maoni ili dada yenu mkubwa awasaidie kujua kipi ni ukweli na kipi ni uzushi.

Share your feedback