Nani anasema kwamba hedhi ni "uchafu"?

Usiamini kila unachokisikia

Kuanza kupata hedhi inaweza kuwa kitu kinachoogopesha, na wakati mwingine ni zile dhana za kizamani zinazosema hedhi ni uchafu. Hili halina ukweli wowote, matokeo yake hutufanya tujisikie wapweke. Ukweli ni kwamba, hedhi inawapata karibia nusu ya watu waishio duniani, na sio uchafu ama kitu cha kukionea aibu. Ukizingatia mambo haya machache yatakusaidia uwe mwenye kujiamini zaidi pindi uwapo katika hedhi na kukufanya kutokuwa na hofu.

1. Hedhi ni sehemu ya maisha yenye afya

Hedhi ni kitu cha kawaida kabisa na hakuna ukweli wowote kwamba hedhi ni uchafu. Ni hakika ya kwamba kuona hedhi ni ishara ya kuwa na afya njema. Ni kitu cha asili katika miili yetu na ambacho watu wengi duniani hukipitia. Ndiyo, hata yule muimbaji wa mziki umpendaye ama muigizaji, mwalimu au mwanasiasa wote wanapitia uzoefu huu. Kuzungumza na marafiki zako kuhusu hedhi kutakusaidia kujiamini zaidi na kutokuhisi upo pekeako. Na unaweza hata kuomba msaada kwa mwanamke unayempenda. Kuwa na marafiki wanawake ambao unaweza kuongea nao itakufanya ujisikie kuwa na msaada.

2. Ni sawa kujiandaa mapema

Kama mawazo ya kupata hedhi ghafla yanakufanya uwe na wasiwasi, sasa kwanini usiwe na vitu unavyovihitaji kwenye begi lako? Weka pedi, vitambaa, na chupi ya ziada hii itamaanisha upo tayari muda wowote. Ni jambo la kawaida kabisa hedhi yako kutokuwa na mpangilio maalum katika miezi ya mwanzo, na hivyo unaweza kuanza kuvaa pedi siku chake kabla ya hedhi kuanza. Ni jambo la muhimu sana kuweka kumbukumbu ya tarehe za hedhi katika kalenda yako hii itakusadia kufahamu mzunguko wako.

3. Hedhi sio kitu cha aibu

Nilipokuwa mdogo, nilivunja ungo nikiwa gengeni nikinunua matunda, ambapo mama mmoja alinigusa begani na kuniambia damu ilikuwa ikinichuruzika maana nilikuwa nimevaa kisketi kifupi Hata hivyo, hakunicheka, ama kunifanya nijione nina tatizo. Alinishika mkono na kunielekeza kilipokuwa choo. Ingawa nilijisikia kuaibika kidogo, lakini ukarimu wake ulinifanya nione sikupaswa kujisikia aibu. Wakati mwingine huwa tunatokwa na damu katika mazingira ya ajabu sana, lakini hatupaswi kuona aibu.

Hivyo kumbuka--hedhi ni hatua nzuri ya kukuandaa kuelekea kuwa mwanamke bora uliyonuiwa kuwa. Hazibadili thamani yako ama kukufanya mchafu. Ni kitu cha kawaida na ni sehemu ya maisha yetu. Na ikitokea watu watajaribu kukusema ama kukufanya ujisikie tofauti simama jitetee na usisahau Kukukumbuka DONDOO hizi.

Share your feedback