Jaribu mambo haya kujipa raha mwenyewe!
Jina langu ni Caroline. Nilikuwa nikichukia sana tukifunga shule maana Likizo ilikua inaboa mno, kwa sababu sikuwa na kitu cha kufanya isipokuwa kumsaidia mama yangu kazi za ndani! Kwa bahati nzuri likizo hii binamu yangu Maria alikuja kututembelea. Maria ni mbunifu sana alinionyesha jinsi ninavyoweza kutumia ubunifu wangu katika kutafuta namna ya kuifurahia likizo lakini pia kuifurahisha familia yangu.
Tengeneza kitabu cha historia ya familia yako
Kitu cha kwanza tulichofanya ni kutengeneza kitabu chenye stori tamu kuhusu familia zetu mfano: Ile ya wazazi wetu wakiwa wadogo walivyokimbizwa na mbwa wakati wanachuma maembe.Unajua Bibi yetu alifariki miezi 6 iliyopita, basi Maria aliona kama hii itakuwa njia nzuri ya kuhakikisha kwamba hatusahau stori zote ambazo aliwahi kutusimulia Kwa hiyo, tulitumia karatasi tulizochana kwenye baadhi ya madaftari yetu na kalamu za wino wa bluu na mweusi tulizopata ndani .Tulivyomaliza kuandika,tukazitoboa karatasi zetu pembeni,tukapitisha kamba ili zikae pamoja kama kitabu.Jamani, ni rahisi sana kufanya! Kwanini na wewe usijaribu?
Cheza mchezo wa alfabeti
Maria pia alinifundisha mchezo wa alfabeti ambao unatakiwa kutaja kitu chochote ambacho kinaanza na kila herufi ya alfabeti, kuanzia mwanzo hadi mwisho. Lakini kila kitu unachokitaja lazima kitoke kwenye kundi moja mfano vyakula, waimbaji, viongozi maarufu waliopita au Nchi mfano Herufi A ni Angola, B ni Burundi nk Tulinogewa kucheza huu mchezo hadi mama akaona na yeye acheze pia.
Kuwa msaada kwa wahitaji
Kuna mambo madogo yana baraka sana zaidi ya kumsaidia mtu mwenye shida tu. Mimi na Maria tulikuwa tukijitolea kwa masaa kadhaa kila wiki katika kituo cha watoto yatima kuwasaidia watoto kusoma na kuandika. Binafsi nilijisikia vizuri sana kuwa wa manufaa kwa watu katika jamii yangu, na hasa kwa kuwasaidia watoto hao kujifunza kusoma na kuandika.
Sasa hivi nafurahia kweli vipindi vya likizo kwa sababu napata nafasi ya kufanya mambo mapya ambayo mwanzo nilikuwa siwezi kufanya maana nilikuwa bizee mnoo na kuchoka pia. Shukrani zangu zimuendee Binamu yangu Maria aliyenitia moyo kuutumia ubunifu nilionao na rasilimali zilizopo katika mazingira yangu!
Share your feedback