Mama katika umri wa miaka 16
Mambo vipi wasichana
Naitwa Khadija na ni mmoja Kati ya watoto 8 toka kwa baba na mama wenye upendo mkubwa sana. Baba yangu alikuwa na kazi hivyo ilitufanya kuishi maisha yasiyokuwa na shida. Lakini siku alipofariki tu maisha kila kitu kiligeuka.
Nchini kwangu, mjane hana haki ya kuendelea kuishi nyumbani kwa mumewe. Hivyo baba zangu kubwa walitulazimisha kuondoka nyumbani na ikatubidi kuondoka kwenda kuishi katika shamba dogo kijijini kwao mama. Nililazimika kutokwenda shule kwa mwezi mzima ili tu kumsaidia mama kufyatua matofali ili tuweze kujenga nyumba mpya. Maisha yetu yalikuwa yale ya kupata mlo mmoja tu kwa siku.
Ilikuwa haijalishi nimechoka au Nina njaa kiasi gani, Mara zote nilijitahidi sana kwenye masomo yangu. Nilijipa moyo na kuendelea kuzingatia masomo. Kila nilipopata muda baada ya kazi za shamba na usafi wa nyumbani nilijitahidi kusoma ili kujiandaa na mitihani yangu ya mwisho ya elimu ya sekondari. Jitihada zangu zilizaa matunda na nilifanikiwa kufaulu vizuri sana. Lakini hatukuweza kumudu gharama za ada. Nilikaa mwaka mzima nikisubiri kurudia mtihani tena nikiwa na matumaini ya kupata ufadhili wa kwenda kusoma shule ya bweni na nilipata..
Siku moja, mmoja wa marafiki niliosoma nao alinishawishi twende bichi, Si nikakutana na kaka mmoja mzuri huyo! . Tokea siku Ile tulianza kuwa tunachati na baada ya muda aliniomba niwe mpenzi wake. Nilimkubalia na tukawa wapenzi. Alinishawishi tufanye ngono, mmh! miezi michache baadae nilipata mimba.
Nilikuwa sijawahi hata siku moja kuongea na mtu yeyote kuhusu ngono. Kiukweli hii hali ilinichanganya sana. Sikujua hata aina gani ya kinga ya kutumia na hata namna ya kutumia, nilimuamini tu angenilinda. Taarifa za kuwa na mimba zilikuwa ni taarifa nzito sana kwangu, taarifa hizi ziliniumiza na zilimuumiza mama yangu pia. Nilikuwa na mpango wa kumaliza elimu yangu lakini mimba ilimaanisha kwamba ndo nimepoteza nafasi yangu ya kufadhiliwa.
Nilipojifungua mtoto wangu wakiume nilijawa na upendo na furaha kubwa kwa sababu nilimleta kiumbe mpya duniani. Maisha bado yalikuwa magumu lakini tuliyamudu. Baada ya mwaka mmoja, mtu mmoja alikuja nyumbani - aliniambia alikuwa anafanya kazi katika shirika la kutoa misaada kuwasaidia vijana, wasichana waliozaa kurudi shule na kupata elimu.
Aliniambia ili niweze kustahili kujiunga nilitakiwa kujitolea kuwa mfundishaji rika na kuwaeleza wasichana wengi stori ya maisha yangu ili waweze kujifunza na kuwahimiza wawe jasiri na kukataa kufanya kitu chochote ambacho hawapo tayari kukifanya. Nilikubali, na nilishukuru kwa kupata nafasi ya kuendelea na elimu na kuwasaidia wasichana wengine kama mimi.
Mwanangu ana miaka 3 sasa hivi. Nimebakiza miaka miwili tu ili kuhitimu elimu yangu ya sekondari. Nimepitia mengi sana na bado stori yangu haijaisha bado. Kuacha shule na kujifungua ni sura mojawapo katika stori ya maisha yangu. Najua kama nitajituma na kufanya kazi kwa bidii bila kukata tamaa hakuna kizuizi kitakachonishinda.
Ingawa watu watanifikiria vibaya kwa kuzaa nikiwa bado mdogo, najivunia kuwa mfano kwa wasichana wengine. Jambo la muhimu ni kwamba nawahimiza wasichana wengine waliojifungua kurudi shule, na kuwashauri wasichana wengine wasibebe mimba wakiwa bado wadogo.
Share your feedback