Kuwa msichana anayejitegemea – sehemu ya 2

Usisimame mpaka ufike kwenye mstari wa ushindi

Mambo vipi msichana,

Hebu kumbuka kile nilichokueleza katika stori yangu iliyopita ya kuwa msichana anayejitegemea sehemu ya kwanza. Anza kwa kujiamini, kama bado hujaisoma nenda chini ya ukurasa huu na chagua sehemu iliyoandikwa "Pia unaunaweza kupenda".

Hata hivyo ni kweli kwamba kujiamini ni ufunguo wa kila kitu. Toka nilipoanza kuwa na mawazo chanya, vitu vizuri vimekuwa vikitokea katika maisha yangu.

Kama vile zile wazo Zuri la biashara nililopata mwezi uliopita. Mimi na bibi yangu tumekuwa tukifurahi kuoka keki pamoja na Mara zote watu wanapotutembelea huulizia keki tunazooka. Hivyo nikajiuliza kwanini tusianze kuuza keki mtaani kwetu.

Mwanzoni lilionekana jambo rahisi sana, lakini kuanzisha biashara yako binafsi sio jambo rahisi hata kidogo. Kuna vitu vingi sana vya kuvizingatia na mambo mengi yanaweza kutokwenda sawa. Lakini nilikumbuka sipaswi kujikita kuwaza mambo mabaya. Ili uweze kujitegemea unapaswa kuamini kuwa haijalishi kitu gani kitatokea katika maisha yako unatakiwa kujua wewe ni imara na unaweza kusimama na kushinda muda wowote.

Nilitamani kuanza kuuza keki katika maduka ya kawaida kabla sijawa na duka langu binafsi. Hivyo nilienda katika duka la mikate lililopo jirani na kumuuliza kama angeweza kuniruhusu kuuzia keki zangu katika duka lake. Alinikubalia na kunipatia pesa ya kununulia bidhaa za kuanzia. Nilikuwa na shauku kubwa sana. Nilikuwa nimepiga hatua moja kuelekea katika kuwa huru na mwenye kujitegemea.

Nilipokuwa njiani kuelekea nyumbani kuanza kazi ya kuoka, boda boda niliyokuwa nimepanda ilizima ghafla. Nilipepesuka na niliangusha vitu vyangu chini. Nilichanganyikiwa kabisa. Nilimuahidi mwenye duka kwamba kesho yake ningempelekea keki lakini sasa kila kitu nilichokuwa nacho kilikuwa kimemwagika na sikuwa na pesa yoyote ile ya kununulia vitu. Sikujua kitu cha kufanya. Nilitaka kukata tamaa. Kwanini maisha yanakuwa magumu hivi?

Nilipokuwa nimesimama pale huku nikiziangalia ndoto zangu za kuwa huru na mwenye kujitegemea zikiwa zimetapakaa pale chini niliisikia sauti ya bibi yangu mawazoni ikiniambia " mawazo hasi hayawezi kukupa maisha chanya" hivyo niliipinga sauti hii hasi na nilianza kujiambia kila kitu kitakuwa sawa. Na wakati huo niliamua kutokukata tamaa na kuwa jasiri.

Yote haya yalinifundisha kuwa njia ya kuelekea kuwa mwenye kujitegemea haijanyooka. Kutakuwa na kupanda na kushuka lakini jambo muhimu songa mbele.

Je unataka kufahamu jinsi nilivyoweza kusimama tena? Soma sehemu ya 3 hapo chini ili kufahamu yaliyojiri...

Share your feedback