Wasichana au wavulana...

Nani mwenye haki zaidi?

Siku ya kwanza tuliporudi shule baada ya likizo, mvulana mmoja wa darasa la juu alimpiga Pendo kofi makalioni. Hii haikuwa mara ya kwanza kwa jambo hili kutokea. Lakini ilikuwa muda wa kukipinga kitendo hiki, kwa wavulana na wasichana ambao hawakumheshimu pale shuleni. Hivyo, Pendo aliamua kupambana na waliokuwa wakimuonea na akawashinda!

Hivi ndivyo alivyofanya!!

Tambua haki zako- Pendo alitambua kuwa tabia hii haikuwa nzuri. Alikuwa akitambua kuwa wasichana Wana haki ya kutokushikwa miili yao na walipaswa kuheshimiwa. Wasichana Wana haki ya kufurahia elimu sawa kabisa na wavulana. Hakutaka kuendelea kukubaliana na majibu ya walimu kwamba "wavulana watabaki kuwa wavulana"

Hamasisha kujitambua - Pendo alikusanya taarifa za wasichana wa darasani kwake na wasichana wengine ambao waliwahi kufanyiwa vitendo hivi katika shule yao. Alishangazwa na wingi wa wasichana waliomueleza kuhusu jinsi walivyokuwa wamekasirishwa na kitendo cha wavulana kuwadhalilisha bila kupewa adhabu yoyote. Aliwashirikisha wazazi wake kuhusu taarifa hizi na wazazi wake waliwashirikisha wazazi wengine na hatimaye taarifa zilifika shuleni.

Usiwasikilize wanaokuchukia - watu watakuzuia usizungumze. Lakini kama kuna kitu kinakukera, au kinakuvunjia haki yako, kukizungumza ni jambo la msingi mno. Kama alivyofanya Pendo. Mara zote unaweza kuzungumza na watu unaowaamini. Dada yako, wazazi, mwalimu au marafiki zako - zungumza na yoyote anayeweza kukutetea. Sikiliza watu wanaokupenda na achana na wanaokuchukia.

Tambua nguvu uliyonayo - Tambua unayo nguvu ya kubadilisha mambo. Usiruhusu watu wakufanye uamini kuwa wavulana ni bora kuliko wasichana. Kila siku, wanawake na wasichana duniani kote wanazibadili jamii zao. Kupitia mambo madogo kama vile kuwajulia watu hali na jinsi wanavyojisikia kunaweza kuleta badiliko kubwa.

Kwa kuzungumza juu ya swala hili , na kusambaza jumbe za sauti za wasichana wengine, Pendo aliweza kuwapa msukumo shule kuweka adhabu kali kwa wavulana wote watakaowadhalilisha wasichana pale shuleni.

Wakati mwingine mtu atakapojaribu kukwambia "wavulana watabaki kuwa wavulana" tambua una haki ya kupaza sauti yako na kupinga. Sio lazima ufanye kama alivyofanya Pendo lakini unaweza kuwasaidia wasichana wengine kwa kupaza sauti zao pale wanapokushirikisha uzoefu wao. Wingi huleta nguvu na kwa pamoja itafanya sauti zenu kuunguruma.

Share your feedback