Rafiki zangu ni washida na raha
Habari! Naitwa Amina, na ninaishi katika mji mdogo karibu na Arusha Tanzania. Nina bahati sana kwasababu nina marafiki wa kweli Neema na Mariam. Kila Jumamosi tunapenda kuenda kuangalia filamu katika kibanda cha kuonyesha video karibu na shuleni kwetu.
Basi Jumamosi moja, mimi na marafiki zangu tulikuwa tunaenda kuangalia filamu na babu muuza duka alimwita Neema. Babu huyo huwa anamsumbua sana Neema sababu mama yake anadaiwa dukani. Mimi na Mariam tuliendelea kutembea taratibu tukijua Neema atatukimbilia. Baada ya dakika tano tuligeuka na kuona Neema akitukimbilia, sura yake ilionekana ina wasiwasi. Neema alinisogelea kwa karibu na kuninong’oneza, Amina unatokwa damu. Neema alinionyeshea chini ya kiuno, na nilipoangalia nikaona doa kubwa jekundu kwenye nguo yangu. Nilikuwa nimeanza siku zangu.
Nilitaka kuanza kulia hapo hapo, lakini marafiki zangu walinipa moyo. “Hamna mtu alioona doa kwenye nguo yako Amina. Lazima wangetuambia. Na pia, hiki ni kitu cha kawaida kwahiyo usione aibu”, alisema Mariam. Neema alikimbia dukani na kuniletea kanga kufunika doa la damu. Na kisha kwenda duka la dawa kuninunulia pedi.
Sisi tulimsubiri Neema chini ya mti. Wakati tunamsubiri, Mariam aliniambia siri kubwa; Mariam alianza kuona siku zake miezi 6 iliyopita. Aliniambia alikuwa anaogopa sana mwanzoni lakini dada yake alimwambia kuwa kupata siku zako ni jambo la kawaida na siyo jambo la kuonea aibu. Mimi na rafiki zangu tulianza kutembea kurudi nyumbani ili niweze kuvaa pedi. Nawashukuru sana rafiki zangu. Neema aliniambia “Amina. Huu sio ugonjwa hutakufa. Ni hali ya kawaida ya kuwa msichana. Usiogope, utakuwa sawa.” Na kweli niko sawa na nina furaha!
Share your feedback