Nilijisikia aibu nilipokuwa shuleni

Sikuwa tayari kwa kile kilichokuwa kinakaribia kunitokea

Mwaka huu nimefikisha miaka 13 na mwezi uliopita nilipata hedhi kwa mara ya kwanza. Nilipoona damu kwenye chupi yangu kwa mara ya kwanza nilishangaa, ila sikuogopa kwa sababu mama aliwahi kuniambia kuwa ntaanza kupata hedhi nitakapoanza kubalehe. Nilimueleza kilichotokea na alinipa boksi la pedi na akanifundisha namna ya kuziweka kwenye chupi yangu. Hili lilikuwa jambo jipya kwangu na ilinichukua muda kulizoea ila baadaye nikalizoea.

Mgeni asiyetarajiwa

Mwezi mmoja baadae nikiwa napata chakula cha mchana na marafiki zangu katika ukumbi wa chakula nilianza kujisikia maumivu ya tumbo. Nilidhani labda nimekula kitu kibaya kumbe ilikuwa dalili kwamba hedhi ilikuwa inaanza na sikuwa nimejiandaa.

Nilihisi damu ikinitiririka miguuni, na nilijua yawezekana sketi yangu ilikuwa imelowana pia. Sikuweza kusimama. Nilijisikia aibu mno. Nilijiuliza kwanini hali hii imenitokea nikiwa kwenye ukumbi wa chakula huku nimezungukwa na watu wengi hivi jamani?

Fedheha? Aibu? Hapana. Haikuwa kitu cha namna hiyo.

Nilitakiwa kwenda nyumbani mapema ili ninawe na kubadilisha chupi. Nilimueleza mama kile kilichojitokeza na nilijisikia kulia kwani niliamini lazima watu waliona kilichonipata. Lakini mama yangu alinipa moyo kuwa sikupaswa kujisikia aibu.

Alisema "Mambo huwa yanaonekana ya aibu kutokana na stori tunazojiambia katika akili zetu." Aliniambia sipaswi kuwaza mambo hasi kuhusu jambo hili. Badala yake napaswa kuwa na mawazo chanya kuhusu kilichotokea. Mawazo kama vile "hedhi ni kitu cha kawaida" na mambo magumu hutokea ila jambo muhimu ni namna unavyokabiliana nayo."

Kuwa muelevu kuhusu hedhi

Mama alinieleza kuwa kupata hedhi bila kutarajia ni kitu cha kawaida kwa wasichana walio wengi katika kipindi cha mwanzo. Unapaswa kuwa muelevu na kuweka kumbukumbu ili kuhakikisha umejiandaa Mara zote.

Mmh! kuweka kumbukumbu? Sikuwahi kufikiria kufanya hivyo. Niliandaa kalenda maalum kwa ajili ya hedhi yangu na kila mwezi nimekuwa nikihesabu siku ya kwanza ninapoona damu ya hedhi kama siku ya 1 na siku 28 zinazofuata kabla ya kupata hedhi nyingine. Kwa wasichana walio wengi hupata hedhi Kati ya siku 21 na 35 hivyo napaswa kubeba pedi kutoka siku ya 21.

Hivyo wasichana, kumbuka hedhi sio jambo la kulionea aibu. Hakikisha Mara zote una pedi na weka kumbukumbu ili uweze kujiandaa. Na hata kama bado mambo yatakuendea vibaya. Usihofu, waza kwa haraka na fanya maamuzi.

Share your feedback