Sina wazazi

Lakini nina haki!

Tanzania ina yatima wapatao milioni 3.1 na karibu nusu yao wamepoteza wazazi wao kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI. Ifuatayo ni stori ya msichana mmoja:

Naitwa Florence, nina miaka 20. Nilipokuwa mdogo niliishi na shangazi na mjomba. Walinifanya niamini kuwa walikuwa na haki ya kunipiga na kunionea kwa sababu sikuwa mtoto wao wa kuzaa, na sikuwa na sehemu nyingine yoyote Ile ya kukimbilia,kiukweli sikuwa na chakufanya.

Walikuwa waonevu sana kwangu. Nilipomuomba shangazi kunipatia pedi wakati nilipopata hedhi alinijibu "si utumie gazeti" nilipohitaji kutengeneza nywele ili nipendeze, alinijibu "Jua na maji vipo nahitaji nini tena? Hali ilikuwa mbaya sana. Maisha yangu yalikuwa magumu sana katika kile kipindi. Nilikatishwa tamaa sana.Pale nilipokuwa nikimaliza kazi za nyumbani usiku ndipo nilikuwa nachukua madaftari yangu ili kufanya mazoezi ya shule.

Siku moja, baada ya kuwaza kwa muda mrefu sana kuhusu swala hili, nilipata ujasiri wa kwenda kuzungumza na afisa jamii ambaye nilisikia habari zake kutoka kwa mmoja wa walimu wangu pale shuleni. Nilikuwa nimejawa na uoga. Lakini nafurahi kwamba niliweza kufanya hivyo. Aliyabadili maisha yangu.

Nilipokwenda kwake nilimueleza stori yangu na nililia sana. Alinitazama machoni na akaniambia, "MWANANGU, HAKUNA MTU anayestahili kukupiga ama kukuonea" aliongozana nami kwenda nyumbani ili kuzungumza na walezi wangu. Alifanya vikao kadhaa. Ilichukua muda lakini hatimaye aliweza kunitafutia sehemu nyingine ya kuishi. Niliweza kuzingatia masomo yangu, na niliweza kuwa jasiri.

Nilipokuwa nikiishi kwa shangazi na mjomba wangu nilikuwa nikiogopa kuomba msaada. Sasa hivi nipo salama na mwenye furaha. Najivunia tena. Mimi ni msichana niliyepigania haki zangu na kushinda.

Share your feedback