… lakini bado natimiza ndoto zangu.
Mambo vipi wasichana!
Naitwa Ruth niliolewa nikiwa mdogo! Nilipomaliza elimu ya sekondari, wazazi wangu walinitafutia mchumba na nikaolewa. Mwanzo ndoa ilikuwa nzuri lakini baada ya muda mambo yalizoeleka kwani yalikuwa yale yale kila siku, unaamka, namsaidia Mume wangu kujiandaa kwenda kazini, kufanya shughuli za nyumbani, kula na hatimaye kurudi kulala.
Mara nyingi nimekuwa nikijiuliza, "Je hivi ndivyo ambavyo maisha yangu yote yatakuwa ama naweza kutimiza ndoto zangu za kuwa mwalimu?"
Siku moja jioni baada ya chakula, nilimpeleka Mume wangu sehemu fulani tuliyoifurahia na ndipo nikamwambia natamani kujiendeleza na kutimiza ndoto yangu ya kufundisha. Alinikatalia alisema ningekuwa na kazi nyingi mno za kufanya. Mazungumzo yalikuwa magumu na tulishindwa kufikia muafaka. Niliamua kutokupiga kelele na kuachana na mabishano.
Hivyo niliamua kupata ushauri kutoka kwa mama. Mara zote amekuwa akinisaidia kila Mara ninapokuwa nataka kufanya maamuzi magumu.
Mama yangu aliniambia ndoa ni jambo gumu na wakati mwingine huwa vigumu kwa wanandoa kuelewana, hasa pale wanawake wanapotaka kutimiza ndoto zao. Alinieleza kwa sababu swala hili lilikuwa la muhimu sana kwangu nilipaswa kuanzisha mazungumzo haya na kumsaidia mume wangu kuona Umuhimu wa mimi kutimiza ndoto zangu. Kwa mfano, nitaweza kuchangia kipato katika Familia yetu, pia nitaweza kuelewa changamoto anazokutananazo kazini kwake na nitaweza kumpa ushauri sahihi. Lakini pia kwa sababu wote tutakuwa na kipato itatusaidia kuweza kutunza pesa kwa ajili ya Familia yetu katika siku zijazo.
Mama alinipa dondoo hizi Tatu za namna ya kukabiliana na mazungumzo magumu.
Hakikisha upo katika eneo tulivu.
Tafuta Mada ambayo itamvutia kila mmoja ili iwasaidie kujenga ukaribu na kurahisisha mazungumzo.
Eleza kile unachokitaka kwa uwazi, hata pale mambo yanapokuwa magumu kumbuka kutokupaza sauti.
Niliufuata ushauri niliopewa na mama. Mume wangu alionekana kutiliamaanani wazo la mimi kufundisha na alisema atalifikiria. Baada ya muda alibadili mawazo yake na kuanza kuniunga mkono kwa nia moja.
Nimetambua kuwa kama bado una ndoto unaweza kuzitimiza, hata kama uliolewa ukiwa mdogo, unapaswa kutafuta mtu sahihi atakayekushauri na kukuunga mkono.
Share your feedback