Kuwawakilisha wasichana wenzangu wote!

Tunaweza kuwa viongozi pia

Je amewahi kutokea mtu yeyote akakwambia kwamba wavulana tu ndio wanastahili kuwa viongozi? Au kwamba wasichana wapo kwa ajili ya kukaa pembeni tu na wasiseme lolote? Basi, ikiwa uliwahi kuambiwa hivyo maisha yako yote, niko hapa kukujuza kwamba si kweli!

Naitwa Selina na ninasoma shule ya mchanganyiko.Kila mwaka kuna nafasi zinazoachwa wazi katika Baraza la Wanafunzi. Hiki huwa ni kikundi cha wanafunzi wanaoshikilia nafasi za uongozi na uwakilishi wa wanafunzi wengine wote wakati wa kufanya maamuzi makubwa. Pia, wakati ule ambapo wanafunzi wanakuwa wana kero, Baraza la Wanafunzi huweza kupeleka kero hizo kwa Mkuu wa Shule.

Kwa muda mrefu nafasi hizo katika Baraza la Wanafunzi zimekuwa zikishikiliwa na wavulana. Wasichana wachache wamejaribu kugombea lakini mara zote wavulana ndio waliochaguliwa. Baadhi ya wavulana walikuwa viongozi wazuri lakini wakati mwingine sisi wasichana tulipokuwa tukiongelea changamoto zinazotughusu , ilionekana kama vile tunapiga tu kelele na hakuna mtu aliyetusikiliza. Hili jamabo lilikuwa linanikera sana. Na ilikuwa inanisumbua sana kichwa changu maana Wasichana na wavulana wote ni sawa na sauti zao zinastahili kusikilizwa.

Mara tu nilipokidhi vigezo, niliamua kugombea nafasi fulani katika Baraza la wanafunzi kwa sababu niliona ni muda muafaka kwa wasichana kuwa na mwakilishi. Mmoja wetu alihitaji kujitosa ili kuwa sauti ya wasichana wengine ambao hawakuwa na fursa ya kujieleza. Na mtu huyo ni MIMI!

Nilipiga kampeni kwa bidii na hatimaye nikapata nafasi!. Mwanzoni, nikiwa msichana peke yangu ilikuwa inaopesha kidogo, lakini nilijua kwamba natakiwa kuwa jasiri kwa vile wasichana wengine walinitegemea. Baada ya mkutano wetu wa kwanza, wavulana walianza kunikubali na kutambua kwamba hata sisi wasichana tunaweza kuwa na mchango mkubwa na kwamba mawazo ya kujenga yanapatikana pale ambapo wasichana na wavulana wakishirikiana kwa pamoja . Sisi wasichana tuna namna ya kipekee ya kufikiria mambo na hivyo maamuzi yanapofanyika ni muhimu tuwepo na kutoa maoni yetu. Si kila mara inabidi kusubiri kupewa nafasi ya kuongea, unatakiwa tu kuongea.

Basi Wasichana kumbukeni – Utakachokisema ni cha msingi sana na wasichana wengine wanakutegemea wewe, kwa hiyo jiamini ! na mara zote hakikisha unapata kilicho haki yako.

Share your feedback