Vunja Ukimya,Upate kile unachokitaka!

Tulianzisha timu ya mpira wa miguu ya wasichana tupu.

Mambo vipi Wasichana!

Naitwa Naomi ninasoma katika shule ya mchanganyiko wa wasichana na wavulana. Tangu nilipokuwa mdogo nilikuwa napenda kucheza na ndugu zangu mpira wa miguu . Lakini nilipoenda sekondari, wakati wa michezo wavulana walikuwa wanaenda uwanjani kucheza mpira ila wasichana walitakiwa kubaki darasani na kujisomea. Nilipomuuliza mwalimu wangu sababu za wasichana kutoweza kucheza mpira wa miguu, alinijibu kuwa"ni mchezo wenye vurugu nyingi" hivyo wasichana hawataufurahia kabisa.

Hebu Fikiria hilo! Unajua Wasichana pia tuna nguvu, na tunaweza kufanya chochote ambacho wavulana wanafanya. Hatutakiwi kubaki ndani kila wakati na kufanya kazi laini laini tuu.Kujishughulisha na kujaribu mambo mapya ni kitu muhimu pia.

Tulipotoka shuleni niliongea na wasichana wenzangu kuhusu swala hili ,Na kumbe hata wao walikuwa na mtazamo kama wangu! Tunaamini kuwa wasichana wana haki sawa na wavulana, tulichohitaji kufanya ni kuungana, na kupaza sauti zetu na kuwa na msimamo maana Umoja ni nguvu.

Kukusanya wachezaji

Tulihitajika kufanya kitu ili sauti zetu ziweze zisikika, hivyo kwanza tulikusanya kila mtu kwa ajili ya majadiliano ya muda mfupi ili kuhakikisha sisi sote tuna lengo moja. Ni muhimu sana kuonekana kama kundi moja wakati wa maamuzi. Baadaye tulikwenda uwanjani ili kucheza mechi ya kirafiki yaani Ilinoga sana!

Safari Inaendelea

Siku iliyofuata habari zilienea kuhusu mipango yetu na ilikuwa habari njema sana. Kadri siku zilivyozidi kwenda ndivyo wasichana wengi zaidi waliendelea kujiunga nasi kila siku baada ya masaa ya shule.Unajua Unapaswa kufanya kitu ili kuwaonyesha watu kwamba unachukulia malengo yako kwa uzito,au kwamba unamaanisha unachokisema. Wanasema maneno matupu hayavunji mfupa. Kwa matendo yetu tulionyesha kwamba wasichana pia wanaweza kucheza michezo pia. Na watu waliweza kujionea wenyewe.

Kufikia lengo letu

Tulipaza sauti zetu. Tulichukua hatua ili kuonyesha nia tuliyokuwa nayo. Hatimaye tuliamua kuandika barua ya maombi kwa mkuu wa shule na kumweleza umuhimu wa mpira wa miguu na michezo mingine kwetu. Mimi ,pamoja na wasichana wengine wawili tulipeleka barua hiyo na kuomba ikiwa tunaweza kuunda rasmi timu yetu baada ya kutoka shule. Pamoja na hayo tuliomba tupatiwe kocha mzuri na mazoezi sawa na wavulana. Unataka kujua nini alichotujibu? Alikubali ombi letu. Aliona shauku na ushupavu wetu na alifurahia sana wazo letu.

Mpaka sasa tumeshinda michuano mingi sana shuleni. Na tumedhihirisha ya kuwa wasichana tunapoungana pamoja , kuchukua hatua na kusema mawazo yetu, tunaweza kuwa na ushawishi juu ya maamuzi yanayotugusa sisi moja kwa moja..

Share your feedback