Jinsi Huyu Mkaka Alivyonisaidia Mambo Yalipoharibikia!
Mambo vipi! Jina langu ni Hadija, nina umri wa miaka 16.Mtaani najulikana na watu wote kama " Msichana anayecheza mpira wa miguu na wavulana". Ni kweli mimi ni msichana peke yangu katika timu ya mpira wa miguu shuleni. Watu huwa wananiuliza kuwa najisikiaje kushindana na wavulana kwenye michezo,Mie huwa nawambia tu kuwa" wasichana wanaweza kufanya mambo mengi ambayo wavulana wanayafanya ikiwa tu wanapewa nafasi."
Timu yetu hufanya mazoezi siku tano kwa wiki,Kwahiyo huwa muda mwingi nautumia nikiwa na wavulana.Huwa tunaongelea mengi kuhusu soka hasa timu tunazozipenda na wachezaji pia, huwa sina cha zaidi hayo ambayo huwa naongea nao. Mtu mmoja tu ambae nina ukaribu naye,anaitwa John,ni jirani yangu lakini pia Mama zetu ni mashosti sana.. Hata hivyo, kuna mambo kuhusu mimi ambayo hata John hayajui. Si unajua tena mambo ya wasichana ambayo hawezi kuelewa eh!
Siku moja, tulikuwa tukifanya mazoezi tukijiandaa kwa ajili mechi dhidi ya timu pinzani.Siku hiyo nilikuwa bize najinoa kwa ajili ya hiyo mechi, mpaka nikasahau kuangalia kalenda yangu kuona lini naingia kwenye siku zangu na ndo kwa bahati mbaya sasa, nikaanza siku hiyo hiyo tukiwa mazoezini John, aliona damu kwenye nguo yangu akaning’ongoneza, "Hadija damu imevujia kwenye nguo yako". Niliogopa, hapo hapo nikakimbia kwenda kwenye choo cha wanawake.ila sasa sikuwa na nguo nyingine ya kubadili wala pedi. Nikawaza, “dah! nitafanya nini sasa?”Mungu si athumani akatokea rafiki yangu Anna hapo chooni huku kabeba nguo za kubadilisha na pakti ya pedi kumbe John alimweleza shida yangu na ndo alieumuagiza aje kunisaidia.
Nilipopata ujasiri wa kurudi uwanjani, nilirudi huku moyoni nikiamini kuwa John na wengine wangenitania tuu..Lakini cha kushangaza sasa ni hiki,nilipofika tu wote kwa pamoja waliniuliza, "Oya Uko tayari kucheza mpira?" Hapo hapo nikaelewa kuwa walaa hakuna hata wa kunitania kwa sababu hedhi ni kitu cha kawaida.,Niliwajibu kwa kutabasamu "Niko tayari kushinda!" kiukweli sijawahi kujisikia aibu tena kuhusu kuwa kwenye siku zangu.
Share your feedback