Ila nina dukuduku moyoni!
Naitwa Janet, hivi karibuni nimehamia mji mpya.Wazazi wangu walihamia hapa kikazi, kwahiyo niliwaacha rafiki zangu na kuhamia shule mpya.
Siku ya kwanza shuleni, nilikuwa na wasiwasi mkubwa wa jinsi ya kutengeneza marafiki wapya, lakini nilikutana na mkaka anaitwa Fred. Wakati wa chakula cha mchana, alinifata na kunialika kwenye benchi alilokuwa amekaa na marafiki zake. Aliniambia mambo yote niliyohitaji kujua kuhusu shule yaani walimu ambao ni wapole,wakali, jinsi ya kuongea na mpishi ili akupe chakula kingi na mahali wanapokaa wababe wa shule. Nilianza kula naye chakula cha mchana pamoja na rafiki zake kila siku na saa zingine tulitembea wote kurudi nyumbani.
Siku moja, tulipokuwa tukitembea na marafiki zangu niliosoma nao darasa moja, msichana mmoja aitwaye Haika aliniuliza, " Hivi ni lini utatuambia kuwa wewe ni mpenzi wake Fred?" nilishituka! Ni kweli kwamba nilikuwa nahisi kumpenda kwa mbali Fred, hata hivyo, hakuwa mpenzi wangu. Nilimuuliza amezipata wapi hizo habari, akaniambia alimsikia Fred akiwaambia marafiki zake walipokuwa kwenye kipindi cha somo la hesabu.
Nilikasirika sana mpaka nikashindwa kuongea hadi mwisho wa safari. Kwanza kabisa, nilitaka nimchunie Fred, lakini nilipomuona wakati wa chakula cha mchana, nilijisikia tu kwamba nilipaswa kusema kile nilichokuwa nakifikiria. Hivyo nilimsogelea akiwa mbele ya marafiki zake, nilimueleza kile nilichokuwa nimekisikia, na niliweka wazi kuwa mimi sio mpenzi wake. Nilimueleza zaidi kuwa kama atashindwa kuwaeleza watu ukweli, urafiki wetu ungekufa.
Alikiri ukweli mbele ya marafiki zake na marafiki zake walimcheka na kumtania mno. Hata baada ya kumueleza haya bado nilikuwa nimemkasirikia. Huwa sipendi mi mtu aniamulie mambo yangu, Nina akili zangu.Kama angeweza kusubiri, nani ajuaye yawezekana tungekuja kuwa wapenzi sasa hivi. Lakini kwa vile alishindwa, ndio ameshapoteza nafasi hivyo.
Share your feedback