Namna ya kuandika wasifukazi mzuri

Unaweza kuwa na wasifukazi mzuri – hata kama hujawahi kuajiriwa

Sio kazi zote huhitaji wasifu kazi au CV, lakini kuna baadhi ya waajiri na watu wanaotangaza kazi huomba wasifu kazi, kwa hiyo ni vizuri kujua jinsi ya kuiandika.

Na hata kama huna uzoefu wowote wa kazi, , usiache hali hiyo ikuzuie kutuma maombi ya kazi. Kuna mambo unayoweza kuyaandika katika wasifu kazi wako ili yakuongezee nafasi ya wewe kuonekana kwa urahisi.

Kumbuka vidokezo hivi sita:

1. Ifanye kuwa rahisi:

Hakuna haja ya kuweka madoido,kuremba maneno au kuweka picha.Tumia tu karatasi nyeupe ambayo haijapigwa misitari na kalamu ya wino mweusi. Kama unaweza kutafuta namna ya wasifukazi wako kuchapwa basi fanya.Ikiwa hujui kutumia kompyuta, nenda kwenye kibanda cha huduma ya intaneti au mwombe rafiki yako akusaidie. Japo ni sawa kuiandika kwa mkono, hakikisha tu kwamba ni safi na hakuna makosa yoyote.

2. Kuwa makini na ujue yanayojiri kila siku:

Hakikisha anwani yako ni sahihi. Ongeza namba yako ya simu (na anwani ya barua pepe ikiwa unayo na unaweza kua unachungulia mara kwa mara kuona kama kuna chochote kilichotumwa). Wasifu kazi humfanya mtu anaeisoma ajenge picha kichwani ya wewe jinsi ulivyo., kwa hiyo hakikisha anwani yako imekaa kitaaluma kwa mfano surangumu@hotmail.com- si njia nzuri ya kujitambulisha mbele ya bosi wako mtarajiwa. Ikiwa unahitaji kuibadilisha au kufungua mpya, tumia mtindo rahisi kama vile jina lako kamili, la katikati au herufi za kwanza za majina yako na jina lako la mwisho.

3. Jitambulishe:

Jumuisha mistari kadhaa juu ya ukurasa umwambie mwajiri wako wewe ni nani na ujuzi mkubwa zaidi ulio nao na hulka zako nzuri( mfano Mchapakazi) Ikiwa unaomba kazi nyingi tofauti tofauti, hakikisha unachukua muda wa kuandika ujuzi ule unaoendana na kazi unayoiomba.

4. Usijaribu kuandika ujuzi wa kazi usiokuwa nao:

Angazia mambo yale uliyowahi kufanya, kama vile kazi za kujitolea, shughuli za kijamii, vilabu ambavyo wewe ni mwanachama. Ikiwa una ujuzi wa kazi ulioupata wakati ukiwa shuleni, ujumuishe. Ikiwa ulifanya kazi za hapa na pale, au umefanya kazi kama kuuza bidhaa sokoni au kuwafanyia majirani kazi, ziorodheshe pia. Ikiwa unaweza, mwombe mtu uliyemfanyia kazi akuandikie barua ya kukupendekeza inayozungumzia tabia zako nzuri.

5. Orodhesha masomo na kozi ulizosoma shuleni:

Andika masomo na kozi zile zinaendana na kazi unayoomba. ziandike hapo juu. Orodhesha mafanikio yako ya kielimu au tuzo ulizopewa. ukielezea matokeo ya utendaji wako katika sehemu hizi zitafaa sana kwa kazi unayoiomba. Barua ya kukupendekeza kutoka kwa mwalimu wako inaweza kukusaidia.

6. Jumuisha vilabu, kamati ulizowahi kushiriki, michezo na shughuli ulizofanya nje ya shule:

Mambo haya huonyesha kwamba u mwanatimu mzuri, na ikiwa ulikuwa na cheo cha mwenyekiti, mweka hazina au katibu katika vilabu au vikundi vya michezo, viandike na ufafanue majukumu na kazi ulizokuwa nazo.

Kuwa Jasiri. Usikate tamaa ya kutafuta kazi unayoitamani na tunakutakia kila la kheri!

Share your feedback