Barua Taka, Ulaghai, Virusi! Ni nini?

Namna ya kuzuia

Mpendwa Bi. Nai,

Unaweza kunifafanulia virusi vya kompyuta ni nini? Je virusi ni sawa na barua taka? Sina uhakika hivi vyote vinamaanisha nini ila ninachojua ni kuwa vyote viwili ni vibaya!

Wako Mwaminifu,

Binti Jijini Dar

Mpendwa Binti Jijini Dar

Virusi vya kompyuta vinaweza kuvamia simu au kompyuta yako kama ugonjwa unavyovamia mwili wako. Virusi kwa kawaida huvamia simu ya mkononi au kompyuta yako bila wewe kujua. Vinaweza kusababisha vifaa vyako kufanya vitu kinyume cha matakwa yako, kama vile kutuma barua pepe kwa jina lako! Virusi vinaweza kufanya kifaa chako kuzimika, kusababisha kupoteza chochote ambacho unaweza kuwa umehifadhi kama vile picha, miziki au magemu.

Virusi kwa kawaida hupitishwa kutoka kwenye kompyuta moja hadi nyingine -- au simu na simu -- kupitia faili au viungo vya mtandao. Kwa hiyo njia bora ya kuzuia virusi kutoshambulia simu ya mkononi au kompyuta yako ni kuepuka kushiriki faili na kufungua viungo vya mtandao au kurasa kutoka kwenye vyanzo vya tovuti zisizojulikana.

Kwa kompyuta yako unaweza kuiwekea kinga ya virusi au programu ya kuzuia virusi. Hata hivyo, wakati mwingine wamiliki wa vituo vya huduma za mtandao kwa malipo hawafanyi hivi na kompyuta zao zinaweza kusambaza virusi. Ulinzi dhidi ya virusi huwa kwa kawaida huwa haupatikani kwenyesimu za mkononi. Kwa hiyo kwa simu ya mkononi, jaribu kuepuka kutima faili kupitia Bluetooth au kubofya anuani za tovuti zinavyoenekana kutiliwa shaka.

Ukiona umepokea kitu kutoka kwa rafiki kwenye Facebook au barua pepe ambacho unaona hakielewek eleweki,basi inawezekana kuwa akaunti yake imeathiriwa na virusi. Ikiwa kiungo au chapisho linaonekana ni la kutiliwa shaka, muulize rafiki yako ikiwa alituma kabla ya kufungua.

Virusi pia vinaweza kusababisha akaunti za mtandao wa jamii au barua pepe yako kutuma "barua taka" kwa marafiki zako wote. Barua taka inamaanisha ujumbe usiofaa uliotumwa kupitia Intaneti kwa watu wengi. Hivi vinaweza kuwa viungo vya ulaghai au matangazo au picha za ngono. Ikiwa kompyuta au simu yako ya mkononi ina virusi, basi virusi vinaweza kuanza kutuma barua pepe taka au ujumbe, na hilo linaweza kuwa jambo la kuaibisha sana.

Kwa hiyo ni muhimu kuwa na uhakika kuhusu kiungo kabla ya kukibofya ili kuepuka kupakia virusi kwenye simu ya mkononi au kompyuta yako. Simu ya mkononi au kompyuta yako ikianza kufanya kazi katika namna isiyo ya kawaida, nenda kwenye duka/stoo ya kompyuta au simu ya mkononi kwa ajili ya kupata msaada haraka iwezekanavyo!

Uwe makinii sana juu ya kile unachokibofya!

Wako Mpendwa, Bi. Nai

Share your feedback