Mmmh! Simtaki bosi wangu kwenye Facebook yangu!

*Mpendwa Bi Nai *

Nimekuwa nikifanya kazi yangu baada ya shule kwa takribani miezi 6, tangu nilipokuwa na miaka 17. Mwezi uliopita nilijiunga kwenye Facebook. Nilipokuwa nikingia kwenye akaunti yangu kazini. Bosi wangu aliniona na akataka kuwa rafiki yangu kwenye Facebook. Huwa haturuhusiwi kutumia simu zetu tunapokuwa kazini, hivyo niliogopa sana kuwa ingeleta msala kama nisingemkubalia. Kimbembe ni hiki sasa hivi ananitumia meseji akiniomba tukutane nje ya kazini. Inanifanya sijisikii poa kabisa jamani nifanyeje? Ninahitaji sana pesa ili kuwasaidia kaka zangu wadogo wasome, na sitaki kupoteza kazi yangu, lakini sipendi anayoniambia.

Wako mwaminifu,

Mfanyakazi mwenye Wasiwasi.

Mpendwa Mfanyakazi Mwenye Wasiwasi,

Ninaelewa vyema haja ya wewe kuisaidia familia yako. Hebu tuone kama tunaweza kupata njia ya kuondokana na hii changamoto. Ni wazi kwamba bosi wako anafanya isivyofaa. Anatumia cheo chake kujaribu kukutumia kwa faida yake, na hivyo si vizuri!

Vitendo vya bosi wako vinaitwa unyanyasaji wa kingono. Anatumia cheo chake ili kukunyanyasa, kwa sababu anafahamu kuwa unaihitaji hii kazi sana. Una haki kisheria kujisikia uko salama popote uendapo, hata unapofanyia kazi pia, hata kama kazi hiyo ni rasmi au isiyo rasmi.

Hatua ya kwanza itakuwa ni ya kuondoa urafiki kwenye Facebook au kumzuia asiangalie facebook yangu. Hiyo inamaanisha kuwa hawezi kuona au kuchapisha vitu kwenye ukurasa wako au kukutumia ujumbe. Ninatumaini bosi wako atapata somo na kukoma vitendo vyake. Ikiwa unahisi una ujasiri wa kutosha, unaweza pia kumwambia moja kwa moja kuwa hujisikii vizuri kutokana na ujumbe wake, na kwamba huna haja.

Endapo hii haitakusaidia, au kama unaogopa kumfata kumueleza basi, zungumza na mtu mzima aneaminika anayeweza kukusaidia kukabiliana na hali hii. Huyu anaweza kuwa mtu mlie nae kazini au nje, kama vile mzazi, mwalimu au rafiki mkubwa kiumri. Ikiwa eneo lako la kazini lina idara ya rasilimali watu, pia unaweza kuzungumza na mtu kutoka idara hiyo na kuwasilisha lalamiko rasmi.

Kumbuka kuwa si kosa lako, na hupaswi kujisikia kuwa na hatia! Kwa msaada wa mtu mzima anaeaminika, unaweza kutatua matatizo. Kama sivyo, unaweza ukaona na kuamua ni bora kuendelea kufanya hii kazi au hii au ukatafute tu nyingine.

Kila heri! Tupo pamoja

Wako Mpendwa Bi Nai.

Share your feedback